Wamiliki wa baa Kiambu washauriwa wajitayarishe vyema
Na LAWRENCE ONGARO
WAMILIKI wa sehemu za burudani zikiwemo baa katika Kaunti ya Kiambu wamepewa hakikisho kuwa biashara zao zitarejelewa kama kawaida lakini waweke mikakati jinsi inavyostahili.
Gavana wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro alisema kabla ya biashara hiyo kurejelewa kama kawaida, ni sharti wafanyabiashara hao waweke mikakati ya kufuata sheria na kanuni za Wizara ya Afya.
“Ni lazima uweke maji ya kunawa mlangoni, wateja walio katika baa wanastahili kuweka nafasi kutoka kwa mmoja hadi kwa mwenzake, na pia ni lazima kuzingatia muda au saa za kuendesha biashara hiyo.
Aliyasema hayo mnamo Jumatano katika hospitali ya Ruiru Level 4, wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa kitengo kingine kitakachokuwa na vitanda 150.
Jambo la kufurahisha wakazi wa Ruiru ni kwamba jengo hilo litakamilika kujengwa kwa muda wa mwezi mmoja pekee huku wajenzi hao wakitumia teknolojia ya kisasa.
“Tunataka kuona tunajiweka chonjo kukabiliana na Covid-19. Tayari tumefikisha kiwango cha vitanda 630 katika hospitali tofauti,” alisema Dkt Nyoro.
Alisema serikali yake imetenga takribani Sh63 milioni kukamilisha mradi huo wa hospitali ya Ruiru.
Aliahidi kwa muda wa mwezi mmoja ujao “tunatarajia kuwa na vitanda 1,200 vya wagonjwa wa Covid-19.”
Alisema katika hospitali ya Tigoni wana hewa ya kutosha aina ya oksijeni ambayo imehifadhiwa kwa mitungi.
Mbunge wa Ruiru, Bw Simon King’ara alisema ni heshima kubwa kujengewa kitengo kingine cha hospitali kwa sababu hadi sasa idadi ya wakazi wa Ruiru imegonga 490,000.
Barabara kuu ya Thika Superhighway imeweka mji wa Ruiru katika ramani ya nchi kwa sababu takribani wasafiri wengi hupitia kwenye barabara hiyo kila siku.
Aliwahimiza viongozi waache kupiga siasa duni lakini wajiunge pamoja ili kutumikia wananchi.
“Huu sio wakati wa kukosana kama viongozi lakini ni vyema kushirikiana pamoja. Kila kiongozi achunge sehemu yake ili wananchi wapate huduma ipasavyo,” alisema Bw King’ara.
Seneta maalum Bw Isaac Mwaura alisema ataendelea kutetea maslahi ya wakazi eneo hilo.
“Bado tutaendelea kusisitiza kuwa ni sharti ugavi wa fedha uzingatie wingi wa watu ili kila mmoja apate haki yake. Kiambu ni sehemu kubwa ambayo inastahili kupewa fedha kulingana na wingi wa wakazi,” alisema Bw Mwaura.
Alisema yeye kama mtetezi wa wanyonge ataendelea kufanya kazi pamoja na viongozi wengine kwa manufaa ya wakazi wote wa Kiambu.
“Wakati huu sisi kama viongozi tuungane pamoja ili tufanyie watu kazi bila kuwabagua kwa misingi ya ukabila. Mji wa Ruiru umebeba makabila ya tabaka mbalimbali,” alisema Bw Mwaura.