• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 11:14 AM
Idadi ya wanaotafuta huduma za upasuaji imeshuka – wizara

Idadi ya wanaotafuta huduma za upasuaji imeshuka – wizara

Na SAMMY WAWERU

WIZARA ya Afya imesema Jumamosi idadi ya wagonjwa wanaotafuta huduma za upasuaji imeshuka kwa kiwango kikubwa tangu janga la Covid-19 liingie nchini.

Akitumia mfano wa wanaotumia bima ya afya ya NHIF kulipia upasuaji, Waziri Msaidizi katika Wizara Dkt Mercy Mwangangi amesema idadi yao imeshuka kwa 10,000 ambapo baina ya Machi na Mei 2020, takwimu zinaonyesha ni wagonjwa 32,717 waliopata huduma ya aina hiyo.

Waziri amesema mwaka huu kabla ya Kenya kuthibitisha kuwa mwenyeji wa corona, idadi ya waliofanyiwa upasuaji kuanzia Januari, kupitia ufadhili wa NHIF ilikuwa imefika wagonjwa 44, 528.

Dkt Mwangangi alieleza hayo wakati akitoa takwimu za maambukizi ya Covid-19 nchini, katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

“Idadi ya wagonjwa wanaotafuta huduma za upasuaji imeshuka kwa kiwango kikuu tangu Covid-19 iingie nchini. Huduma za upasuaji zingali zinaendelea nchini,” akasema.

Upungufu wa wagonjwa wanaotafuta huduma za matibabu na upasuaji umeonekana kuchangiwa na hofu ya wagonjwa kupimwa ili kujua ikiwa wana ama Covid-19 au la, kabla ya kuhudumiwa.

Aidha, Dkt Mwangangi amethibitisha kwamba iwapo mgonjwa anayetafuta huduma za upasuaji haonyeshi dalili za Covid-19 hapimwi homa hiyo.

Wakati huo huo, Mkuu wa Afya ya Umma, Dkt Francis Kuria amewahimiza madaktari wa upasuaji kuhakikisha wanapimwa Covid-19 kabla ya kuwahudumia wagonjwa.

Afisa huyo pia amesisitiza haja ya kuvalia vifaa vya kujikinga kuambukiza au kuambukizwa corona; PPE.

“Huduma za upasuaji zinaendelea kutolewa katika hospitali husika kote nchini. Kwa madaktari, kabla ya kuhudumia mgonjwa, hakikisha uko salama, fanya vipimo vya Covid-19 na uvalie vifaa vya kujikinga corona,” akashauri Dkt Kuria.

Jumamosi, katika kipindi cha saa 24 zilizopita, imebainika baada ya sampuli kufanyiwa vipimo kwamba watu 515 wanaugua Covid-19. Idadi hiyo inafikisha jumla ya visa 29,849 za waliopatikana na ugonjwa huo tangu kisa cha kwanza kithibitishwe Machi 13, 2020.

Wizara ya Afya pia imetangaza kwamba wagonjwa 672 wamepona chini ya saa 24 zilizopita ikifikisha 15,970 jumla ya waliopona huku wagonjwa saba wakifariki.

Idadi jumla ya waliofariki kutokana na Covid-19 sasa ni 472 nchini.

You can share this post!

Uhuru awapa mawaziri likizo

Equity na kaunti ya Murang’a wajadili ushirika wa Sh5...