Habari Mseto

Wizara yangu ilipokea Sh3b kati ya Sh48b – Kagwe

August 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe Jumatatu aliwaambia wabunge kwamba Wizara yake ilipokea asilimia 15 pekee ya Sh47.9 bilioni zilizotengwa na serikali kufadhili mpango wa kupambana na Covid-19.

Bw Mutahi aliwaambia wanachama wa kamati ya bunge la kitaifa kuhusu afya kwamba Hazina ya Kitaifa ndiyo inaweza kutoa maelezo kamili kuhusu namna sehemu kubwa ya fedha hizo zilitumika.

“Wizara yangu haiwezi kujibikia Sh47.9 bilioni zilizotengwa na serikali kwa ajili ya vita dhidi ya Covid-19 kwa tulipokea sehemu ndogo zaidi ya pesa hizo,” Bw Kagwe akaambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Murangá Bi Sabina Chege.

Bw Kagwe alikuwa ameandamana na Katibu katika Wizara hiyo Bi Susan Mwachache.

Katibu huyo alisema Wizara ya Afya ilipokea Sh3 bilioni ambayo ni sehemuj ya bajeti ya ziada ya Wizara ya Afya na itatuma kwa Hospitali mbalimbali nchini kufadhili maandalizi ya kuwahudumia wagonjwa wa Covid-19.

Miongoni mwa hospitali hizo ni Hospitali Kuu ya Pwani iliyopokea Sh500 milioni, Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH) iliyopokea Sh400 milioni, Hospitali ya Kitui (Sh300 milioni), Hospitali ya Mandera (Sh300 milioni).

Hospitali zingine zilizofaidi ni Hospitali Kuu ya Kenyatta, KNH (Sh600 milion), Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (Sh400 million) na Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (Sh500 milion.)

Bi Mwachache aliongeza kuwa Wizara ya Afya pia ilipokea Sh1.5 bilioni kutoka Hazina ya Kitaifa ambazo zilielekezwa kwa Mamlaka ya Usambazaji Dawa Nchini (KEMSA) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kupima corona na dawa na kutumika katika shughuli hiyo, inayojulikana kwa kimombo kama ‘reagent’.

“Zaidi ya hayo, Wizara ilipokea Sh300 milioni zilizopewa KEMSA kwa ajili ya ununuzi wa barokoa kwa makundi ya watu wenye mahitaji maalum,” Bi Mwachache alisema.

Afisa huyo pia aliongeza kuwa Sh200 milioni kutoka Hazina ya Kitaifa zilitolewa kufadhili utoaji huduma katika vituo vya karantini ambako watu wanaoshukiwa kuwa na virusi vya corona walikuwa wakizuiwa.

Waziri Kagwe alisema uchunguzi unaendelea kuhusu sakata ya ununuzi wa dawa na bidhaa za kimatibabu katika halmashauri ya KEMSA pamoja na bidhaa za kimatibabu zilizotolewa kama msaada na Wakfu wa Jack Maa.