Suala la mpaka wa kaunti lazua tofauti kati ya wazee
GITONGA MARETE Na ALEX NJERU
MZOZO unatokota kati ya Kaunti za Meru na Tharaka-Nithi, baada ya wazee wa baraza la Njuri Ncheke eneo la Imenti Kusini kupinga pendekezo la wenzao wa Tharaka Nithi kwamba mpaka wa kaunti hizo mbili uhamishwe kwa kilomita saba ndani ya kaunti ya Meru.
Mnamo Jumatatu wiki jana, mwenyekiti wa tawi la Tharaka-Nithi la baraza hilo, Bw Kangori Rithaa alisema walikuwa wakijadili na wenzao wa Meru kuhakikisha mpaka umehamishwa hadi Mto Mutonga kutoka soko la Keeria uliopo kwa wakati huu.
“Mpaka kati ya maeneobunge ya Maara na Imenti Kusini ulikuwa Mto Mutonga na ili kuhakikisha wakazi wa pande zote wanatangamana, tunafaa kusuluhisha mzozo huo sasa,” alisema Bw Rithaa.
Alidai kwamba mpaka huo ulibadilishwa wakati wa uongozi wa magavana Peter Munya na Samuel Ragwa baada ya Bw Munya kuweka bango kuonyesha mpaka ulikuwa soko la Keeria.
Hata hivyo, mwenyekiti wa tawi la Imenti Kusini la Njuri Ncheke Bw David Gituma alipuuza madai hayo akisema wazee hao walikuwa wakijitafutia makuu. Alisema mpaka wa kaunti hizo haujawahi kuwa Mto Mutonga, kama alivyodai Bw Rithaa.
“Mpaka haujawahi kuwa Mto Mutonga. Kwa hivyo anayetoa madai hayo anaota mchana. Hatutaki watu wanaotaka kujipendekeza kwa wanasiasa kupanda mbegu za chuki kati ya watu wanaoishi mpakani,” alisema Bw Gituma.