Wakazi Nyali wagomea barakoa wakidai viongozi ni wafisadi
Na DIANA MUTHEU
BAADHI ya wakazi katika eneo bunge la Nyali kaunti ya Mombasa wamesusia kuvalia barakoa wakidai kuwa viongozi wa kisiasa nchini wanatumia janga la corona kujitajirisha.
Wakizungumza katika hafla moja katika eneo la Bombolulu, ambapo wahudumu wa afya ya umma walikuwa wakihamasisha wakazi kuhusu janga la corona, wakazi hao waliwataka viongozi kukomesha ufisadi unaoendelea nchini.
Wengi wao walisema huwa wanavalia barakoa wanapowaona maafisa wa polisi tu ili wasikamatwe.
“Tunavalia barakoa kuifurahisha serikali tu. Ufisadi ambao umekithiri wakati huu unasikitisha. Mwananchi wa kawaida anaendelea kuumia, ilhali kuna watu wanaendelea kujichumia pesa bila kujali,” alisema Bw Wycliffe Mogire ambaye anamiliki kibanda cha mboga.
Mhudumu wa bodaboda aliyejitambulisha kama Leonard aliwataka viongozi kusambaza barakoa kwa watu wote.
“Wakati wa uchaguzi, wanasiasa hawa huleta kofia, shati na hata pesa za bure. Kwa nini wasifanye hivyo msimu huu wa janga la corona ilhali tunasikia katika vyombo vya habari kuwa vifaa hivyo vililetwa nchini kama msaada?aliuliza Bw Leonard.
Afisa wa afya ya umma, Bw James Zuri alisema kuwa ni muhimu watu kuchukua jukumu la kujikinga na maradhi ya Covid-19.
Alisema kuwa baadhi ya wakazi wa Mombasa wanapuuza hatua zilizowekwa na Wizara ya Afya, wakihatarisha maisha yao na watu karibu nao.
Bw Zuri pia aliwaonya wakazi dhidi ya kusambaza habari za uongo kuhusu janga hilo.
“Kwa muda huu kuna changamoto mingi lakini ni vyema tujikinge. Wengine wanasema kuwa janga la corona limekwisha. Corona bado ipo, na ni wajibu wetu kuelimisha jamii wafuate maagizo yanayotolewa na wizara ya afya,” akasema.
Mshirikishi kutoka shirika la The United Front ambalo linashirikiana na kaunti hiyo kuhamasisha watu kuhusu janga hilo, Dkt Suleiman Mwamburi alisema kuwa watatafuta mbinu za kupata barakoa, ili wanapowahamasisha wakazi, pia waweze kusambaza kifaa hicho ambacho ni muhimu wakati huu.