• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Ruto, washirika wakomoa ODM ‘kutetea’ ufisadi

Ruto, washirika wakomoa ODM ‘kutetea’ ufisadi

BENSON MATHEKA Na ONYANGO K’ONYANGO

NAIBU Rais William Ruto amekemea chama cha ODM cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kwa kutetea wizi wa pesa za kukabiliana na corona.

Mnamo Jumamosi chama cha ODM kupitia Katibu Mkuu Edwin Sifuna kilimlaumu Dkt Ruto kwa matamshi yake kuhusu kashfa hiyo alipotaka waliohusika kuchukuliwa hatua.

Bw Sifuna pia alilaumu vyombo vya habari akisema vilikuwa vikiongeza chumvi habari kuhusu sakata hiyo huku pia akitilia shaka uhalisia wa waliofichua sakata hiyo.

Katika ujumbe aliotundika kwenye akaunti yake ya Twitter mnamo Jumapili, Dkt Ruto alifokea na kukejeli ODM kwa kugeuka watetezi wa ufisadi.

“Msimamo wa [uliokuwa] upinzani ambao sasa umegeuka kuwa makuhani wa ufisadi wa kujaribu kutetea wizi wa pesa za covid-19 sio wa kushangaza. Unathibitisha hofu ya Wakenya kwamba upande wao wa handisheki haukunuia kutetea maslahi ya raia lakini ilikuwa nafasi ya kupora. Aibu,” Ruto aliandika.

Alisema msimamo wa ODM unathibitisha viongozi wake ni watu wa kujifanya. Kauli yake ilijiri saa chache baada ya washirika wake kulaumu ODM kwa kuwasulubisha Wakenya kwa kutowaunga mkono kutaka serikali kuonyesha uwazi katika matumizi ya pesa za umma.

Ingawa chama hicho kimekuwa kikiunga serikali tangu handisheki ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, hakijaamua iwapo kitajiunga rasmi na serikali. Ushirikiano huo umekifanya chama hicho cha chungwa kunufaika na nyadhifa za uongozi katika kamati za bunge na seneti kufuatia kuondolewa kwa wandani wa Naibu Rais William Ruto hatua inayoonyesha Bw Odinga ana ushawishi mkubwa serikalini.

Naibu Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee Caleb Kositany alilaumu ODM kwa kutokuwa na msimamo thabiti kuhusu ufisadi. Akihutubia wanahabari nyumbani kwake mjini Eldoret, mbunge huyo wa Soy alisema ODM kiliamua kushirikiana na serikali ya Jubilee kutetea maslahi ya Bw Odinga na sio ya wananchi. Bw Kositany aliwataka viongozi wa chama hicho kueleza Wakenya walivyonufaika na sakata ya Shirika la kusambaza vifaa vya matibabu (Kemsa).

“Kwa miaka mingi, ODM kimekuwa kikijigamba kuwa ndicho chama kinachofichua ufisadi nchini, lakini leo hii hakitetei uovu huu pekee bali pia kinashiriki kuwapora Wakenya. ODM kinafaa kuonyesha kwa vitendo kinapiga vita ufisadi. Tafadhali waeleze Wakenya viongozi wa ODM walipata kiasi gani katika kashfa hii ya Kemsa,” alisema Bw Kositany.

Mbunge huyo alidai kwamba wabunge wawili wa ODM na Seneta wa Trans-Nzoia Michael Mbito walinufaika na sakata ya Kemsa lakini chama hicho kimenyamaza.

“Ni lazima ODM itue leze kwa nini Seneta wa Trans-Nzoia ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya afya ya seneti alifanya biashara na Kemsa na kwa nini hii ilitumiwa kumshinikiza kuunga kutimuliwa kwa Kindiki Kithure (Tharaka Nithi) kutoka wadhifa wa Naibu spika wa seneti,” Bw Kositany alidai bila kutoa ushahidi wowote.

Seneta Mbito alikanusha madai ya washirika wa Dkt Ruto kwamba alishinikizwa kuunga kutimuliwa kwa Bw Kindiki akiyataja kama propaganda.

“Sio kweli, ni propaganda. Nilifanya uamuzi wangu binafsi kuunga ajenda za Rais,” Bw Mbito alisema.

“Naelewa kwa nini Katibu Mkuu wa ODM alitetea wanaofyonza waathiriwa wa corona katika Kemsa. Kwanza, ODM wanafikiri ndio serikali kuliko Jubilee. Pili, wanachama wanne wakuu wa ODM ndio wale wafanyabiashara ambao hawakufichuliwa katika sakata ya Kemsa,” Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen alisema kwenye ujumbe wa Twitter.

Mnamo Jumamosi, ODM kupitia Katibu Wake Mkuu Edwin Sifuna kilimlaumu Dkt Ruto kwa kujitenga na kashfa vya Kemsa.

Dkt Ruto alikuwa amesema kwamba hawezi kulaumiwa kwa sakata hiyo kwa sababu ametengwa serikalini.

You can share this post!

Bayern Munich yapiga PSG 1-0 na kutwaa ufalme wa UEFA

Vyuo vikuu MKU na Leipzig cha Ujerumani, vyafadhili watafiti