• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 1:13 PM
Wafaa kunishukuru, Muthama ajibu Kalonzo

Wafaa kunishukuru, Muthama ajibu Kalonzo

Na GASTONE VALUSI

SENETA wa zamani wa Machakos, Johnson Muthama, amejibu madai ya kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kuwa amekuwa akimwelekeza njia zisizofaa za kisiasa.

Bw Muthama alikejeli kauli hiyo ya Bw Musyoka, na kusema inamfanya aonekane kuwa mtu asiyeweza kusimama imara anapojiunga na mirengo ya kisiasa.

Akijibu kauli ya Bw Musyoka kuwa alishurutishwa na yeye (Muthama) kujiunga na mrengo wa Raila Odinga mara mbili, seneta huyo wa zamani alisema amefurahi kuwa ametambuliwa kama kigogo wa siasa za Ukambani.

“Mimi ni dume kamili kama ninao uwezo wa kumbeba Makamu wa Rais na kumpeleka pahali ambapo hataki. Nimefurahi sana kwamba ananitambua kuwa kigogo wa siasa za eneo hili,” akasema.

Mnamo Ijumaa, akiwa nyumbani kwa kigogo wa zamani wa siasa za Ukambani, marehemu Mulu Mutisya, Bw Musyoka alidai kuwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2013 na 2017, alishurutishwa na Bw Muthama kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga.

“Naapa kuwa sitakubali Muthama anishawishi tena kuwa mgombea mwenza wa mtu yeyote. Nitafanya uamuzi wangu mimi mwenyewe kuhusu hatima ya maisha yangu ya kisiasa,” akasema Bw Musyoka.

Lakini Bw Muthama aliyezungumza Jumamosi kijijini Mbilini, Kangundo kwenye mazishi ya Masaku Ngei, mwanaye mpigania-uhuru, waziri na kigogo wa siasa wa zamani marehemu Paul Ngei, alisema Bw Musyoka si mtu wa kujituma kisiasa.

“Anapaswa kunishukuru badala ya kunikashifu. Kama si kupitia juhudi zangu, Kalonzo hangepata wadhifa wa Makamu wa Rais. Ni mimi nimekuwa nikimsukuma kufanya kazi na Raila,” akasema.

Gavana wa Nairobi, Mike Sonko aliwataka viongozi wa Ukambani wakomeshe uhasama kati yao, akisema uadui wao utaikosesha jamii ya Wakamba kiti cha urais mwaka wa 2022.

“Ninawaomba viongozi wote katika eneo hili kuweka kando tofauti zao na kuungana kutatua shida za wakazi kama vile umaskini, maji, huduma za afya na masomo badala ya mashindano yasiyo na msingi,” akasema Bw Sonko.

You can share this post!

Achoshwa na dhuluma za kimapenzi, awatilia wazazi sumu

Afisa wa DCI azimwa kumumunya hongo