• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Kaunti yaanza kuchunguza ardhi zilizotolewa kwa umma kiharamu

Kaunti yaanza kuchunguza ardhi zilizotolewa kwa umma kiharamu

Na VALENTINE OBARA 

SERIKALI ya Kaunti ya Kisumu imeanzisha uchunguzi kuhusu ardhi za umma zilizotolewa kwa wawekezaji kupitia njia haramu.

Jopokazi lililobuniwa na Gavana wa kaunti hiyo, Prof Anyang’ Nyong’o, litahitajika kuchunguza jinsi ardhi za umma zilivyonyakuliwa na watu binafsi tangu enzi za utawala wa mabaraza ya miji yaliyosimamiwa na mameya na kutoa mapendekezo kuhusu hatua inayostahili kuchukuliwa.

“Watahitajika kutoa ripoti ambayo itaongoza Serikali ya Kaunti ya Kisumu kwa ushirikiano na Tume ya Kitaifa ya Ardhi kutwaa ardhi za umma ambazo zilitolewa kinyume na sheria, nyumba za serikali, vyeti vya kukodisha ardhi za umma na mitaa iliyo Kaunti ya Kisumu,” ikasema taarifa ya kaunti iliyochapishwa katika baadhi ya magazeti jana.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza jopokazi kama hilo kubuniwa kwani kumewahi kuwepo mengine katika miaka iliyotangulia, ingawa hakujapatikana mafanikio kutatua unyakuzi wa ardhi uliotendeka kufikia sasa.

Kutokana na hali hii, serikali ya kaunti ilisema jopokazi lililochaguliwa litahitajika pia kutathmini ripoti zilizotolewa awali kuhusu unyakuzi wa ardhi na kutoa mapendekezo kuzihusu.

Serikali hiyo ilitoa agizo kuzuia uuzaji wa ardhi zinazolengwa kufanyiwa uchunguzi kuanzia sasa hadi wakati uchunguzi utakapokamilika. Agizo hili linahusu pia ardhi zilizopeanwa kwa watu binafsi na baraza la mji wa Kisumu lililokuwepo katika mwaka wa 2010.

Baadhi ya ardhi ambazo zilinyakuliwa kutoka kwa umma ziko mjini Maseno, mitaa ya Kanyakwar, Kibos, Migosi, Mamboleo na Dunga.

Wananchi walitakiwa kuwasilisha maoni au malalamishi kuhusu ardhi za umma zilizonyakuliwa kwa jopokazi hilo kuanzia Mei 14 hadi Juni 8, mwaka huu kibinafsi au kupitia kwa makundi.

Malalamishi yote yatahitajika kuambatishwa na stakabadhi husika.

You can share this post!

Onyo kwa waundaji wa filamu bila leseni

USM Alger yatua nchini kukabiliana na Gor Confederations Cup

adminleo