Habari Mseto

Maraga adai Uhuru amepuuza utekelezaji Katiba

August 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

JAJI MKuu Jaji Maraga anasema Kenya ina Katiba nzuri zaidi duniani lakini utekelezaji wake usioridhisha unaifanya isinufaishe wananchi walioipigania kwa miaka mingi.

Akizungumza kwenye mahojiano na runinga ya NTV Jumapili usiku, Bw Maraga alisema ni jukumu la Rais Uhuru Kenyatta kutekeleza Katiba ya nchi.

“Ilipopitishwa 2010 nilidhani ulikuwa mwanzo mpya kwa sababu mambo mengi yalikuwa yameenda kombo na watu wengi walidhani ulikuwa mwamko mpya,” akasema.

“Ikiwa katiba ina kifungu kuhusu haki na hakuna mfumo wa kutekeleza haki hizo, basi katiba hiyo haina makali. Katiba ikiwa na mambo mema ambayo hafuatwi basi haina makali.”

Bw Maraga ambaye anatarajiwa kustaafu Januari 15, 2021, baada ya kutimiza umri wa miaka 70, alisema ingawa bunge lina jukumu la kutunga sheria na Mahakama kutafsiri sheria hizo, ni serikali kuu chini ya Rais inayofaa kuhakikisha Katiba inatekelezwa.

Alishangaaa kuwa wanasiasa huchagua sehemu wanazotaka kutekeleza kwa lengo la kujinufaisha.

“Rais Kenyatta alikuwa Rais wa kwanza kuchaguliwa chini ya Katiba mpya na utekelezaji wa Katiba hiyo ulitwikwa serikali yake,” akasema.

Mnamo Juni 1, 2020, alipoongoza sherehe za Madaraka Dei, Rais Kenyatta ambaye anahudumu kwa kipindi cha pili alisema anaona wakati wa kubadilisha Katiba kurekebisha makosa ambayo walioiandika walifanya.

Wanaharakati wanasema Katiba ya sasa inafaa kutelelezwa badala ya kufanyiwa marekebisho. Kwamba mageuzi ya Katiba yanalenga kufaidi watu wachache wenye ushawishwi.

“Wakenya wengi huheshimu sheria. Ni watu wachache serikalini wanaokaidi na hii imefanya baadhi ya raia kuiga mfano wao,” akasema.

Alieleza hofu kuwa hali hii ikiendelea inaweza kutumbukiza Kenya katika ghasia. Ingawa amekuwa akitofautiana mara kwa mara na Rais Kenyatta, Bw Maraga alisema hana uhasama wa kibinafsi na kiongozi wa nchi.

“Shida yangu ni utekelezaji wa mamlaka ya Ofisi ya Rais,” alisema.

Maraga ambaye aliongoza Mahakama ya Juu kufuta uchaguzi wa urais 2017 ambao Rais Kenyatta alikuwa ametangazwa mshindi, alisema hajuti kufikia uamuzi huo.