Habari Mseto

MKU kutumia mtandao katika sherehe ya kufuzu kwa mahafali Oktoba

August 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

WANAFUNZI wa wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) waliokamilisha utafiti katika kozi mbalimbali wanajiandaa kufuzu kwa awamu ya 18 itakayoendeshwa mnamo Oktoba 9, 2020, kupitia huduma za Intaneti.

Chansela wa chuo hicho Profesa John Struthers, alisema kufuatia hali ya janga la corona hapa nchini, mahafali hao watalazimika kufuatilia mpango huo kupitia mtandao.

Sherehe za hapo awali zilikuwa ni za mkusanyiko wa mahafali, wazazi, wahadhiri na hata wageni waliohudhuria kushuhudia kufuzu kwa wahitimu wa chuo hicho, katika uwanja mkuu wa Graduation Pavallion eneo la Landless, Thika, lakini kutokana na Covid-19, mambo mengi yamebadilika.

Baadhi ya wale wanaotarajiwa kufuatilia hafla hiyo mtandaoni ni wale waliokamilisha tafiti zao katika viwango vya uzamifu, uzamili, shahada ya digrii ya kwanza, diploma, na hata cheti cha stashahada; yaani certificate.

Hapo awali mwenyekiti na mwanzilishi wa chuo hicho, Profesa Simon Gicharu, alikuwa akiongoza hafla hizo katika uwanja wa chuo hicho, huku vituo vya televisheni kadha vikiangazia matukio hayo mubashara.

Hata hivyo hayo yote hayatakuwepo tena kutokana na sheria, ushauri na kanuni zilizotolewa na Wizara ya Afya zikiwemo kupiga marufuku watu kukusanyika pamoja ili kuzuia kuambukizana virusi vya corona.

Kutokana na mabadiliko hayo, wahitimu na wazazi pamoja na jamaa zao watalazimika kufuatilia mtandaoni matukio yote ya kufuzu.

MKU ni kimojawapo cha vyuo vikuu ambavyo vimejitolea kutumia teknolojia ya mtandao ili kuwatunuka vyeti mahafali wake.

“Kwa niaba ya kamati ya muungano ya chuo na seneti, tungetaka kuwajulisha ya kwamba kufuzu kwa wanafunzi kwa awamu ya 18 kutaendeshwa mnamo Oktoba 9, 2020, kupitia mtandao kutoka saa tatu za asubuhi,” ni ujumbe uliotumwa kwa tovuti ya chuo hicho ulionakiliwa na Profesa Struthers.

Ujumbe huo unaendelea kusema ya kwamba majaribio ya maandalizi ya siku hiyo ya kufuzu kwa mahafali yatafanywa mnamo Oktoba 8, 2020.

Wanaoendesha mipango hiyo wanasema ya kwamba watazidi kufuata maagizo ya Wizara ya Afya wakati huo.

Kulingana na Profesa Struthers, ujumbe unaoambatana na hafla hiyo unaeleza: “Kukumbatia teknolojia kwa njia ya kidijitali katika masomo ya juu kwa mafanikio, licha ya changamoto zilizopo.”

Alisema orodha kamili ya wahitimu watarajiwa imechapishwa katika tovuti ya chuo hicho, ambapo wale watakaokosa kuona majina yao kwenye orodha hiyo wameshauriwa wawasiliane na wakuu wa idara na vitengo mbalimbali.

Tovuti hiyo ni https://studentportal.mku.ac.ke

Alisema majina ya wahitimu watarajiwa yatakayoorodheshwa katika tovuti ni ya wale tu ambao tayari wamekamilisha karo yote ya chuo.

“Wahitimu watarajiwa ambao wangeashiria kubadilisha majina yao ili yaambatane vilivyo katika vyeti vyao, wanastahili kuwasilisha stakabadhi zao za chuoni,” wanashauriwa.