• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Sonko aruhusiwa kusuluhishia nje ya mahakama kesi ya ufisadi wa Sh357 milioni

Sonko aruhusiwa kusuluhishia nje ya mahakama kesi ya ufisadi wa Sh357 milioni

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Kaunti ya Nairobi Mike Sonko na washukiwa wengine 16 wameruhusiwa kushauriana na mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) kwa lengo la kusuluhishia nje ya mahakama, kesi ya ufisadi wa Sh357 milioni dhidi yao.

Akitoa mwelekeo kuhusu kesi hiyo, hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Dougkas Ogoti amesema Jumatano “washukiwa wako huru kuanzisha mashauriano na DPP wasuluhishe kesi hiyo nje ya mahakama.”

Wakati wa mashauriano hayo na DPP washtakiwa wanaweza wakapewa fursa ya kurudisha pesa wanazodaiwa walipokea kwa njia isiyofaa kisha kesi inayowakabili itamatishwe.

Na wakati huo huo Bw Ogoti amefahamishwa mmoja wa washtakiwa, Patrick Mwangangi amefariki.

Wakili aliyemwakilisha mshtakiwa huyo ameomba mahakama ifutilie mbali kesi dhidi yake.

“Nachukua fursa hii kuieleza mahakama mshtakiwa wa tatu Patrick Mwangangi alifariki. Tayari amezikwa. Naomba mahakama itamatishe kesi dhidi yake,” wakili George Kithi amemweleza Bw Ogoti.

Hakimu amekabidhiwa cheti cha kifo cha Patrick Mwangangi.

Bw Ogoti ameamuru afisi ya DPP ithibitishe habari hizo na kuwasilisha ripoti Septemba 25, 2020.

Akitoa maelekezo baada ya kufahamishwa na mawakili Mabw Cecil Miller na Kithi wanaomwakilisha Sonko kwamba wamepokea nakala zote za mashahidi, Bw Ogoti ameamuru kesi ianze kusikizwa mbele ya hakimu mwandamizi Bi Kagure Nyutu kila siku hadi itamatishwe.

Mawakili wakiwa kortini. Picha/ Richard Munguti

Bw Ogoti amesema mawakili hawataruhisiwa kujiondoa katika kesi hiyo ikianza kusikizwa.

“Washtakiwa hawataruhusiwa kubadilisha wakili kesi ikianza. Endapo mshtakiwa anataka kubadilisha wakili, lazima iwe siku saba kabla ya kesi kuanza kusikizwa,” amesema Bw Ogoti.

Pia amesema agizo hilo litawalenga mawakili pia.

DPP ameagizwa awasiliane na mawakili wanaowatatea washtakiwa kuhusu shahidi atakayeitwa siku saba kabla ya siku ya kusikizwa.

Sonko na washtakiwa hao 15 wamekanusha mashtaka dhidi yao na wako nje kwa dhamana.

Sonko yuko nje kwa dhamana ya Sh15 milioni pesa taslimu.

You can share this post!

KAFYU: Pigo kwa wenye vilabu vya densi na makahaba

LISHE: Cinnamon rolls