HabariVideo

Sikuiba moyo wa mfu, mpasuaji ajitetea

May 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA mpasuaji mkuu wa maiti wa Serikali Dkt Moses Njue alifikishwa kortini Jumanne kwa kuiba moyo wa maiti katika Mochari ya Lee , Nairobi.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Hali aliwasilisha mashtaka matatu dhidi ya Dkt Njue ya kuiba moyo wa mfu kwa lengo la kulemaza kesi iliyonuiwa kushtakiwa.

Daktari huyo wa kupasua maiti alifunguliwa mashtaka pamoja na mwanawe Dkt Lemuel Anasha Mureithi Njue ambaye hakufika kortini Jumanne alasiri.

Mshtakiwa alikanusha mashtaka matatu ya kuiba moyo, kuharibu ushahidi na kuondoa kiungo katika maiti na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000 pesa tasilimu.

Alishtakiwa kuiba moyo kutoka kwa maiti ya Timothy Mwandi Muumba iliyokuwa imehifadhiwa katika chumba cha Lee.

Na wakati huo huo hakimu mkuu Mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi alitoa kibali cha kumwagiza Dkt Lemuel Anasha Mureithi Njue afike kortini kabla ya siku kusikizwa kwa kesi hiyo mnamo Julai 3, 2018 kujibu mashtaka hayo matatu.

“Namwamuru mshtakiwa wa pili (Lemuel) afike kortini aitha Mei 28 ama kabla ya Julai 3, 2018 kujibu mashtaka,” aliamuru Bw Andayi.

Juhudi za Dkt Njue kupitia kwa mawakili wake kupinga asishtakiwe ziligonga mwamba baada ya Bw Andayi  kutupilia mbali ombi la kutaka kesi hiyo iahirishwe hadi Mahakama kuu itakaposikiza na kuamua ombi  lililowasilishwa na jamaa wa marehemu.

Lakini ombi hilo lilipingwa vikali na wakili wa Serikali Bi Cathertine Mwaniki aliyesema kuwa kesi iliyowasilishwa mwaka wa 2016  ilipania kushinikiza afisi ya DPP ichunguze kisa hicho.

“Uchunguzi ulifanywa na kitengo kinachotokana na mizozo ya kinyumbani katika afisi ya Mkurugenzi wa Jinai (DCI). Ilibainika baada ya uchunguzi kwamba moyo wa  Timothy Mwandi Muumbo kama inavyosemekana katika cheti cha mashtaka,” alisema Bi Mwaniki.

Mahakama ilifahamishwa kuwa mshtakiwa alitiwa nguvuni baada ya polisi kufahamishwa maiti ya Timothy haikuwa na moyo.

Katika kesi iliyowasilishwa katika mahakama kuu walalamishi waliwashtaki Dkt Njue, Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Joseph Boinnet na mwanasheria mkuu  Jaji Paul Kihara ndio wanaoshtakiwa.

“Mashahidi wakiongozwa na Bw Billy Mbuvi wameandika taarifa kutoka kwa mashahidi wote itakayotegemewa na DPP,” alisema Bi Mwaniki.

Kiongozi huyo wa mashtaka alipinga ombi la mshtakiwa akisema walioorodheshwa kutoa ushahidi dhidi yake wameandikisha taarifa kwa polisi.

“Naomba hii korti ikatalie mbali ombi la mshtakiwa na kuamuru ajibu mashtaka,” alisema  Bi Mwaniki.

Hakimu alikubaliana na Bi Mwaniki kwamba hakuna sababu zozote za kuwezesha mahakama kusitisha kushtakiwa kwa Dkt Njue.

Video