• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
Gavana Mwangi wa Iria apigwa faini ya Sh500,000

Gavana Mwangi wa Iria apigwa faini ya Sh500,000

Na MARY WANGARI

GAVANA wa Murang’a amejipata mashakani baada ya Kamati ya Seneti kumpiga faini ya Sh500,000 kwa kukosa kuhudhuria vikao vyake kujibu maswali kuhusu matumizi ya fedha za umma.

Kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari mnamo Ijumaa, Agosti 28, 2020, Kamati ya Seneti kuhusu Fedha za Kaunti na Uwekezaji ilisema kuwa ilichukua hatua hiyo kufuatia kile ilichotaja kama juhudi za gavana huyo “kutatiza kazi ya Kamati.’

“Kamati hivyo basi imeamua kwamba kuambatana na Kifungu cha Sheria 19 (1) kuhusu Kanuni na Mamlaka ya Bunge, Gavana wa Murang’a amepigwa faini ya Sh500,000 kwa kukosa kujiwasilisha baada ya kuitwa na Kamati,” kilisema kijisehemu cha taarifa hiyo.

Kamati hiyo ilieleza kwamba licha ya kumwandikia bosi huyo wa kaunti ikimwalika katika vikao vyake katika tarehe tofauti mnamo Juni, Julai, Agosti na Septemba, bado alikataa kujiwasilisha.

Kupitia mwenyekiti wake Sam Ongeri, Kamati hiyo ilieleza kwamba ilichapisha notisi kuhusu vikao hivyo vya Kamati ya Seneti lakini Wa Iria akakosa kujiwasilisha ili kujibu maswali kutoka kwa afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Vitabu vya Fedha.

Aidha, Bw Ongeri alisema kuwa mwanasiasa huyo alikataa kufika katika vikao vya awali akitaja kiwango cha juu cha maambukizi ya Covid-19 katika Kaunti ya Murang’a, kilichokuwa kimesababisha afisi za kaungti kufungwa, kupitia barua aliyoandika mnamo Agosti 25, 2020.

Hata hivyo, Kamati hiyo ilipuuzilia mbali sababu za Wa Iria ikizitaja kama hila za kutatiza utendakazi wa Kamati hiyo pamoja na kuepuka kuwajibikia matumizi ya fedha za umma.

“Gavana na usimamizi wake walikuwa na notisi na wakati wa kutosha kujiandaa kwa kikao na kwamba kamati inaona notisi iliyotolewa na Wizara ya Afya katika Bunge la Kaunti hiyo, ilikuwa juhudi za kutatiza kazi ya kamati na jaribio la Gavana kutafuta sababu za kutowajibikia fedha za umma,” ilisema.

Mashaka ya Wa Iria yamkini yalianza kufuatia ripoti ya Mkaguzi Mkuu kuhusu rekodi za matumizi ya fedha za umma kiasi cha zaidi ya Sh24bilioni katika kipindi cha 2014/2015 – 2017/2018.

Kamati hiyo imesisitiza nia yake ya kuona suala hilo limesuluhishwa kikamilifu ikisisitiza kwamba wakazi wa Kaunti ya Murang’a wana haki ya kupata uwajibikaji kamili kuhusu matumizi ya fedha zao kutoa kwa kiongozi waliyemchagua.

You can share this post!

Wakazi 500 wa Nyali wanufaika na bima ya afya kutoka mfuko...

Mooy ajiengua Brighton na kuhamia China kuchezea Shanghai...