• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 7:55 AM
Wafanyabiashara walalama bidhaa za kuuza yakiwemo mazao kuteketezwa Githurai

Wafanyabiashara walalama bidhaa za kuuza yakiwemo mazao kuteketezwa Githurai

Na SAMMY WAWERU

MAMIA ya wafanyabiashara wanaouza vyakula na mazao ya kutoka shambani katika soko Githurai wanakadiria hasara kubwa baada ya mali yao kuteketezwa na moto Jumamosi.

Walioathirika ni wanaoendesha biashara karibu na reli. Kulingana na wachuuzi tuliozungumza nao, bidhaa zao ziliteketezwa chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa usalama, ambao hawakuwa wamevalia sare.

Shughuli hiyo imefanyika siku mbili baada ya vibanda na maduka yao kubomolewa kwa matingatinga, Shirika la Reli nchini likiendelea na maandalizi ya harakati za kufufua usafiri na uchukuzi wa garimoshi kati ya Nairobi na Nanyuki.

Baada ya ubomozi huo, wamekuwa wakiuzia bidhaa zao juu ya vyandarua na magunia yaliyotandazwa ardhini.

“Unyama huo ulitekelezwa wakati baadhi yetu tukianza kufungua biashara. Serikali ndiyo inatuhangaisha, sidhani kuna mtu binafsi anayeweza kutufanyia uyama kama huu. Wengi wamepata mali yao yamechomwa. Juhudi zetu kusimamisha uharibifu huu hazikuzaa matunda, maafisa ambao hawakuwa na sare walituonyesha bastola,” akalalamika mchuuzi aliyeomba kubana jina lake.

“Jioni baada ya kazi, huwa tunafunga bidhaa zinalalama humu chini ya ulinzi wa kibinafsi. Juzi walitubomolea vibanda, leo wametuchomea mali, hii serikali haina utu,” akaongeza.

Alisema walitishiwa, maafisa waliosimamia shughuli hiyo wakidai “amri imetoka juu”. “Rais Uhuru Kenyatta ametupuuza, tulimchagua 2013 na 2017 mara mbili, hii ndiyo shukrani yake?” mchuuzi huyo akaelezea ghadhabu zake, akisema ubomoaji wa soko hilo la bidhaa za kula na mazao umeingizwa siasa.

 

Wachuuzi wanaouza bidhaa; hasa vyakula na mazao Githurai – karibu na reli – wanakadiria hasara kubwa baada ya mali yao kuchomwa mapema Jumamosi, Agosti 29, 2020, chini ya ulinzi wa maafisa wa polisi ambao hawakuwa wamevalia sare rasmi. Picha/ Sammy Waweru

 

Mfanyabiashara aliyesema anafahamika sokoni kwa jina Kamaa aliambia Taifa Jumapili kwamba wakati wa tukio, hali ilikuwa ya mguu niponye.

“Hatukuweza kuokoa bidhaa zetu, maafisa hao hawakutaka kuona yeyote akinusuru chake,” Kamaa akasimulia.

“Jana (juzi) nilimwaga machungwa yenye thamani ya Sh22,000, nilikuwa nimefanya mauzo ya Sh5,000 pekee. Ni unyama na aibu serikali kutuhangaisha kipindi hiki ambapo ugonjwa wa Covid-19 unaendelea kutuathiri kwa njia hasi,” akateta mama mmoja akikadiria hasara.

Ubomoaji wa vibanda na maduka yaliyoko karibu na reli eneo hilo, ulifanyika usiku wa kuamkia Jumatano.

Wafanyabiashara walioathirika walilalamikia kupewa ilani ya muda mfupi kujipanga kuondoka.

Baadhi ya wafanyabiashara tuliozungumza nao wanasema Gavana wa Kiambu James Nyoro aliwatembelea baadaye, ila hakuwatatulia masaibu yao.

Ubomoaji sawa na huo pia ulifanyika eneo la Mutindwa, kwa wanaoendeshea biashara kandokando mwa reli.

You can share this post!

Matumaini visa vya corona nchini vikipungua

JAMVI: Mfumo wa ugavi pesa za kaunti wageuka mtihani mgumu...