• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Washirika wa Ruto wakata tamaa kumnasa Mudavadi

Washirika wa Ruto wakata tamaa kumnasa Mudavadi

Na SHABAN MAKOKHA

UTATA kuhusu ni nani atayakekuwa mgombea-mwenza wa mwenzake kati ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi, umefanya wandani wa Dkt Ruto kukata tamaa.

Wawili hao wametangaza azma ya kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, na Bw Mudavadi amesisitiza hataki kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto.

Wandani wa Naibu Rais katika eneo hilo sasa wameamua kumshauri Dkt Ruto kutafuta mshirika mwingine wa kisiasa eneo hilo.

Wakiongea nyumbani kwa mbunge wa Matungu, Justus Murunga mnamo Jumamosi, viongozi hao walioshirikisha aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Dkt Boni Khalwale na mbunge wa Mumias Mashariki, Benjamin Washiali walisema wamejaribu kumshawishi Bw Mudavadi bila mafanikio.

“Ukimtongoza msichana awe rafikiyo kwa miezi sita bila mafanikio, jambo la busara ni kumtafuta msichana mwingine. Tumekuwa tukijaribu kumwomba Bw Mudavadi kukubali pendekezo letu bila mafanikio. Hatuna lingine ila kutafuta mshirika mwingine,” akasema Bw Washiali.

Hata hivyo, alimwambia Bw Murunga kujaribu kumzungumzia Bw Mudavadi kwa mara ya mwisho kabla yao kumtafuta mshirika mwingine kuwa mgombea-mwenza wa Dkt Ruto.Dkt Khalwale alisema Bw Mudavadi amekuwa akibadilisha msimamo wake nyakati tofauti.

“Hakubali uhalisia uliopo kwamba hatafaidika kwa vyovyote vile ikiwa atashirikiana na washindani wetu. Amekuwa akitarajia kwamba atateuliwa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta. Namwambia Bw Mudavadi, kama mtu wa rika langu kuwa jamii ya Abaluhya haitakungoja ili kushirikiana na Dkt Ruto. Itashirikiana naye ukiwepo ama usipokuwepo kwani lazima maisha yaendelee,” akasema Dkt Khalwale, aliyeonekana mwenye ghadhabu.

Bw Wanyama alimrai Bw Mudavadi kupanua mtazamo wake kisiasa kwa kujiunga na Dkt Ruto, aliyemtaja kuwa mmoja wa wagombea wakuu wa urais kwenye uchaguzi wa 2022.“Acha kuzunguka tu katika maeneo ya Vihiga, Busia na Kakamega pekee.

Badala yake, panua mtazamo wako kisiasa,” akasema. Hata hivyo, Bw Murunga alipuuzilia mbali kauli hizo, akisema ataendelea kumshawishi Bw Mudavadi kujiunga na kambi yao.

“Kwa kutofanya uamuzi wa haraka kujiunga nanyi, hilo halimaanishi amekataa kujiunga na Dkt Ruto. Tunapaswa kumpa muda wa kutosha. Bado kuna matumaini,” akasema.

Alieleza kuwa kiongozi huyo anafanya mashauriano ya kutosha kabla ya kufanya uamuzi wake wa mwisho.Alisema licha ya kuwa mbunge aliyechaguliwa kwa tiketi ya ANC, anashirikiana na Dkt Ruto ili kuwaletea watu wake maendeleo.

You can share this post!

Kampuni 8 zilitumiwa kuchafulia Raila sifa 2013 na 2017

Kanisa Katoliki lapinga refarenda ya kujali wachache