Siasa

Ikulu inaingilia ugavi wa fedha za kaunti, Kang'ata afichua

August 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

HUENDA muafaka kuhusu suala tata la mfumo wa ugavi wa fedha miongoni mwa serikali 47 za kaunti usipatikane hivi karibuni baada ya kubainika kuwa Ikulu imewasilisha “mapendekezo yake” kuhusu suala hilo.

Kiranja wa wengi katika Seneti Irungu Kang’ata Jumatatu alithibitisha madai hayo lakini akaondoa hofu kwamba msimamo huo utavuruga mchakato wa maridhiano unaoendeshwa na kamati ya maseneta 12.

“Kuna matumaini kwamba tutapata mwafaka kuhusu suala hili licha kwamba serikali pia imewasilisha msimamo wake kwa uongozi wa Seneti. Hiyo ni sawa. Memoranda hiyo itashughulikiwa pamoja na ripoti kielelezo ambayo kamati hiyo imewasilisha kwetu kama uongozi,” akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge.

Hata hivyo, Bw Kang’ata ambaye ni Seneta wa Murang’a alidinda kufichua mapendekezo yaliyomo kwenye memoranda kutoka Ikulu akisema “hiyo haina maana wakati huu”.

“Ripoti ya kamati hiyo ya maridhiano sasa itajadiliwa katika “Kamukunji” au katika kikao rasmi cha seneti, pamoja na mapendekezo mengine ibuka kutoka kwa wadau wengine,” akaeleza.

Akiongea katika uwanja wa KICC alipotoa hatimiliki 38,000 ya ardhi kwa wakati wa maeneo ya Embakasi na Korogocho Rais Uhuru Kenyatta alijitenga na vuta nikuvute kuhusu ugavi wa fedha kwa kaunti lakini akahimiza kuwa kaunti zote zitendewe haki.

“Kaunti zenye idadi kubwa na watu na zile ambazo zinadhaniwa kuwa zimepiga hatua kimaendeleo pia zina watu masikini na zinapasa kupewa fedha za kutosha. Baadhi ya wakazi wa Nairobi pia wangali wanatumia vyoo vya karatasi za plastiki na wanahitaji fedha za kuimarisha hali zao,” akasema Rais Kenyatta.

Hii ni baada ya serikali kulaumiwa kufuatia kukamatwa kwa maseneta Cleophas Malala (Kakamega), Steve Lelengwe (Samburu) na Christopher Lang’at (Bomet) kutokana na msimamo wao wa kupinga mfumo uliependelea kaunti 29 zenye idadi kubwa ya watu ambazo zimeongezewa mgao wa fedha.

Wiki jana wenyeviti wenza wa kamati hiyo ya maridhiano maseneta Moses Wetang’ula (Bungoma) na Johnstone Sakaja (Nairobi) walisema kamati hiyo imepiga hatua kubwa na “tunakaribia kupata muafaka”.

Hata hivyo, maseneta Samson Cherargei na Ledama Ole Kina, ambao ni wanachama wa kamati hiyo, jana walisema muafaka bado haujafikiwa