• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Hofu pombe ikizidi kuua wakazi Kisii

Hofu pombe ikizidi kuua wakazi Kisii

Na Wycliffe Nyaberi

UTENGEZAJI pombe ya kienyeji umeongezeka katika maeneo kadhaa Kaunti ya Kisii, na kusababisha ongezeko la vifo na mauaji.

Walevi wengi wamegeukia maeneo yanayouza chang’aa baada ya serikali kufunga baa kote nchini katika juhudi za kuzuia msambao wa corona.

Ingawa serikali iliahidi kukabili pombe haramu, bado utengenezaji huo unazidi kukita mizizi na kuchangia vifo vya watu wanne katika maeneo ya kuuza chang’aa.

Mmoja kati ya wanne hao waliuawa ni afisa wa Nyumba Kumi aliyepigwa na bintiye mtengenezaji pombe baada ya mzee huyo kuandamana na chifu kwenye operesheni ya kuharibu pombe yao mwezi Juni mwaka huu katika kijiji cha Mashauri.

Mnamo Mei, mwalimu wa shule ya msingi aliuawa kufuatia sababu kama hizo katika kijiji cha Nyosia.

Mwalimu huyo alikwenda kujistarehesha kunakouzwa chang’aa lakini hakurejea.

Mauaji ya hivi punde yaliyowaghasi watu wengi yalitokea wiki moja tu iliyopita. Mwashi wa miaka 40 alichinjwa kijijini Kenyoro-Etangi, tarafa ya Kiogoro.

Ilisemekana mwashi huyo, Edward Omwamba aliuliwa na mmiliki mmoja mwenye kuuza chang’aa baada ya kuzozana kuhusu deni walilokuwa wakidaiana.

Siku chache tu kabla ya uhamisho wake kwenda Uasin- Gishu, aliyekuwa kamishina wa kaunti ya Kisii Stephen Kihara aliitaja tarafa ya Kiogoro kama mojawapo ya sehemu zenye ngome kuu za utengenezaji wa pombe haramu ambazo zafaa kuangaziwa.

Ni katika mazishi ya Edward Omwamba hiyo jana ambapo viongozi mbali mbali walichukua fursa ya kukemea watengenezaji wa pombe haramu na kumwomba kamishina mpywa Bw Abdirizak Jaldesa kulivalia njuga swala hilo.

Wakiwa na matumaini ya mwakilishi huyo mpya,waombolezaji mmoja baada ya mwingine, hasa kina mama walimwomba Bw Jaldesa kuwaokoa waume na watoto wao kutoka kwa minyororo ya chang’aa ili wawe na kizazi siku zijazo.

“Tafadhali sikieni kilio chetu na nyinyi serikali mkomeshe pombe haramu kwani wanetu wanapotea.Tusipoziba ufa tutakuja kujenga ukuta,” akasema Bi Jane Nyangenya, mmoja wa waliohutubu.

Mwenyekiti wa Nyumba Kumi Kisii Bw Stephen Onsare alidokeza kuwa iwapo pombe hiyo haitakomeshwa, basi jamii itajitokeza na kuwafurusha watengenezaji hao.

“Tumevumilia vya kutosha. Ni wakati sasa kuiga jinsi watu wengine wamefanya ili kukomesha jambo hili ambalo limekuwa sasa dondasugu. Tutahamasisha watu na kwa sauti moja, tutawafurusha wote wanaotengeneza na kuuza pombe haramu iwapo hawatatusikiza,” akasema mwenyekiti.

Zaidi, wenyeji waliomba haki itendeke kwa wote ambao wamepoteza maisha yao kwa kuuliwa kwenye maeneo ya pombe hiyo.

You can share this post!

Msaada wa corona haukuibwa, Kagwe sasa asema

Onyo kwa wakazi wa Pwani wanaouza miti na makaa kiholela