Onyo kwa wakazi wa Pwani wanaouza miti na makaa kiholela
Na MISHI GONGO
SERIKALI imewaonya wanaoendeleza biashara haramu ya kuuza makaa na kukata miti ovyo katika eneo la Pwani.
Akizungumza na Taifa Leo mshirikishi wa usalama katika eneo la Pwani Bw John Elungata alisema ukataji huo umechangia pakubwa katika kubadilika kwa hali ya hewa na uhasama kati ya binadamu na wanyama.
Mkuu huyo alisema shughuli hiyo inaendelezwa zaidi katika kaunti za Lamu, Kwale, na Kilifi.
Alisema kuwa kuendeleza biashara na shughuli za ukataji miti ovyo kutalemaza ari ya Rais Uhuru Kenyatta ya kurudisha asilimia 10 ya misitu ifikapo mwaka 2022.
“Japo serikali imekuwa ikipinga ukataji holela, kuna baadhi ya watu ambao bado wanaedeleza shughuli za ukataji miti. Tutawaandama wanaopuza onyo hili na kuwachukulia hatua,” akasema.
Alitaja maeneo ya baadhi ya sehemu za Kilifi, Lunga Lunga, Samburu na Puma kuwa maeneo sugu ya watu wanaoendeleza biashara hiyo.
“Wakazi wanaoishi katika sehemu kavu za kaunti hii ndiyo wanaendeleza biashara hii. Tutahakikisha kuwa anayekamatwa anachukuliwa hatua kali ili kudhibiti biashara hii haramu,” akasema.
Alisema kuendeleza ukataji miti misituni kunakosesha wanyama wa porini makazi na chakula hivyo kuvamia vijiji na mashamba kujitafutia chakula na hata makazi.
“Tumekuwa tukipokea visa vya watu kuharibiwa mazao yao na wanyamapori au hata kushambuliwa, hali hii inatokana na binadamu kuharibu makazi ya wanyama hawa,”akasema.
Alisema janga la ugonjwa wa Covid-19 nalo limechangia katika kunoga kwa biashara hiyo akisema kuwa wengi ya walioachishwa kazi katika hoteli wamejitosa katika biashara za makaa kujipatia riziki.
“Baada ya serikali kusimamisha kutua kwa ndege kutoka mataifa ya kigeni, sekta ya utalii ilipata pigo kubwa mno. Hoteli zililazimika kupunguza wafanyakazi ili kujimudu. Hali hiyo ilisababisha watu wengi kukosa kazi,” akasema.
Wakati huo huo aliwaonya wahudumu wa bodaboda kwa kukubali kutumika katika kuendeleza biashara hiyo.
Alisema kufuatia uwezo wake wa kupita vichochoroni wachomaji makaa hutumia boda boda hizo kusafirisha makaa yao ili kukwepa mitego ya maafisa wa serikali.
Awali wazee wa Kaya Tiwi walilalamikia kuwa ukataji wa miti umeharibu sehemu zao za matambiko.
Bw Kassim Mnyeto aliiomba serikali kuingilia kati na kuwakamata wanaohusika na ukataji huo akisema kuwa ukataji huo umekuwa tishio kwa kaya zao.
“Msitu huu unaumuhimu mkumbwa kwa jamii yetu. Ni sehemu hii ambayo tunatekeleza maombj yetu. Si sawa msitu huu kukatwa, tunaomba usaidizi wa serikali,” akasema.
Aidha alisema anahofia kuwa miti ya kale itapotea iwapo serikali haitawachukulia hatua wanaotekeleza shughuli hiyo.