Jiandaeni kwa ukame, wafugaji waambiwa
Na COLLINS OMULO
IDARA ya Utabiri wa Hewa nchini imewaonya wakazi wa maeneo ya kaskazini na kusini mwa nchi kuhusu uwezekano wa kupoteza mifugo wao kutokana na kupungua kwa malisho.
Kwenye utabiri wake kuhusu hali ya hewa mwezi huu, idara ilionya kwamba maeneo hayo yataendelea kushuhudia hali kame.
Ilieleza kwamba maeneo ya Marsabit, Isiolo, Wajir, Mandera na Garissa katika eneo la kaskazini yatakumbwa na hali hiyo, sawa na maeneo ya Machakos, Makueni, Kituo na Taita Taveta.Maeneo mengine yatakayoshuhudia hali kame ni Kajiado na Narok.
Hivyo, wenyeji wameshauriwa kujitayarisha mapema, ili kuepuka hali ambapo mifugo wao watafariki kutokana na ukosefu wa malisho ya kutosha.
Mwezi uliopita, maeneo hayo yalishuhudia hali kame zaidi nchini, huku yakipata mvua ya kiwango cha chini ya milimita 20.
Maeneo ya Wajir, Mandera na Voi hayakurekodi mvua yoyote.Kwa mujibu wa utabiri huo, maeneo mengi nchini yatakumbwa na hali kame.
Ni maeneo yaliyo karibu na Bonde la Ufa na Ziwa Victoria pekee yanayotarajiwa kupata mvua chache.
Eneo la Pwani pia linatarajiwa kupata mvua chache nyakati za asubuhi, huku maeneo ya Kati na Nairobi yakipata mvua chache na mawingu mengi nyakati za alasiri siku za mwanzo mwezi huu.
“Inatarajiwa kwamba sehemu kadhaa nchini zitakuwa kame mwezi huu. Hata hivyo, kuna uwezekano mvua ya kiwango cha wastani ikashuhudiwa katika maeneo yaliyo karibu na Ziwa Victoria na maeneo ya juu magharibi mwa Bonde la Ufa,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa idara hiyo Bi Stella Aura.
Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua hiyo Bonde la Ufa ni Trans Nzoia, Kericho, Bomet, Nandi, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Kisii na Nyamira.
Idara ilisema huenda mvua ikaandamana na ngurumo za radi.Hali kama hizo zinatarajiwa kushuhudiwa maeneo ya Kisumu, Homa Bay, Migori, Siaya, Busia, Nakuru, Narok, Baringo na eneo la magharibi Kaunti ya Laikipia.
Mvua chache na hali za mawingu nyakati za alasiri zitashuhudiwa katika kaunti za Nyeri, Murang’a, Kiambu, Kirinyaga, Nyandarua, Embu, Meru, Tharaka Nithi na Nairobi.
“Kuna uwezekano mafuriko kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo yaliyo katika nyanda chini eneo la Ziwa Victoria na maeneo yaliyo karibu na maziwa mbalimbali Bonde la Ufa. Vile vile, kuna uwezekano maporomoko ya ardhi yakatokea maeneo yaliyo nyanda za juu mashariki mwa Bonde la Ufa,” ikaeleza idara.
Mwezi uliopita, maeneo hayo yalipokea mvua kubwa, hali iliyofanya shule kadhaa katika Kaunti ya Baringo kufungwa baada ya maji katika Ziwa Baringo kuvunja kingo zake.
Hali hiyo pia imeshuhudiwa katika maziwa ya Nakuru na Bogoria.