• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 AM
Kilimo cha karakara kimemsaidia kufukuza uhawinde

Kilimo cha karakara kimemsaidia kufukuza uhawinde

Na SAMMY WAWERU

Ili kuwa na afya na kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya mradhi watalaamu wa masuala ya afya wanahimiza umuhimu wa kula matunda mara kwa mara.

Wanapendekeza katika ratiba yako ya mlo kila siku, usikose kuwa na tunda au matunda. Haijalishi iwapo ni matunda ya msimu au ni yasiyokosa sokoni kufuatia jithada za wakulima wanaoyazalisha mfululizo, hususan waliokumbatia mfumo wa kunyunyizia mimea na mashamba maji kwa mifereji.

Bora yawe ni matunda, kwani matunda yanapigiwa upatu kuimarisha kinga ya mwili kwa sababu ya kusheheni Vitamini, madini muhimu katika kudhibiti na kuzuia magonjwa mbalimbali.

Huku matunda yakishabikiwa kutokana na manufaa yake tele kiafya, pia yana faida kwa wanaoyakuza, ndio wakulima.

Kati ya orodha ya matunda, kuna haya yanayojulikana kama karakara. Ukizuru mengi ya masoko nchini, utagundua kwamba kuna uhaba wa matunda hayo kwa sababu si wakulima wengi wanayakuza.

Wachache wanaoyalima kwa msingi wa kilimobiashara hutabasamu wakielekea benkini wakati wa mavuno. Kimsingi, ni zao linaloweza kukutajirisha chini ya muda.

Korir Kandie ambaye ni mkulima wa karakara, mwaka huu wa 2020 ukiwa mwaka wake wa tatu tangu aingilie uzalishaji wa matunda haya, anaungama yana faida tele. Isitoshe, hayana ugumu wowote ule kuyapanda ikiwa mkulima ana kiini cha maji ya kutosha kuyanawirisha.

Barobaro huyu aliingilia kilimo cha karakara 2018, kwa mtaji wa Sh10, 000 pekee. “Umuazi wa kulima karakara niliufanya baada ya kuchoshwa na kazi ya kuajiriwa, ambayo mapato yake yalikuwa ya chini mno,” Korir anadokeza.

Akiwa mhitimu wa Stashahada ya Habari na Teknolojia (IT), kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia (JKUAT), Korir, 25, anaiambia ‘Taifa Leo’ kuwa baada ya kufuzu 2015 na kuhangaika kwa muda, hatimaye alipata kazi kama mhudumu wa mitambo ya mawasiliano katika kampuni moja ya ulinzi jijini Nairobi, mshahara kwa mwezi ukiwa Sh25, 000.

“Maisha jijini Niarobi si rahisi, gharama ya matumizi ilizidi kwa kiwango kikuu mapato yangu,” kijana huyo anaelezea. Ni katika harakati za kutafuta njia mbadala kupiga jeki mapato yake alikutana na rafikiye wa kitambo, anayesema alimfichulia kwamba kilimo cha karakara kimekuwa kikimtia tabasamu. “Aliniambia aliacha kazi iliyokuwa ikimlipa zaidi ya Sh100, 000 kwa mwezi ili kufanya ukulima wa karakara,” Korir anasema.

Kijana Kandie Korir ni mkulima wa karakara Kaunti ya Uasin Gishu, akiwa na mmoja wa mteja wake wakifanya mavuno. PICHA/ SAMMY WAWERU

Ni mzaliwa wa Kaunti ya Uasin Gishu ambapo anasema kwao wamejaaliwa mashamba makubwa, anayosema hulimwa mahindi, ngano na maharagwe msimu mmoja kwa mwaka.

Kwa idhini ya mamake, mnamo 2018 Korir aligeuza ekari moja kuwa kiunga cha karakara. “Mtaji wa Sh10, 000, kutoka kwa akiba yangu, kiasi kikubwa nilitumia kununua miche,” anasema. Kulingana na wataalamu wa masuala ya kilimo, ekari moja inasitiri kati ya miche 800 – 1, 000, na Korir anasema kila mche aliuziwa kati ya Sh8 – 10, tofauti hiyo ikijiri kwa sababu alinunua kutoka kwa wazalishaji miche tofauti.

“Baada ya upanzi na kuitunza, 800 ndiyo ilifanikiwa,” mkulima huyo akafichua wakati wa mahojiano. Mikarakara inachukua muda wa miezi sita pekee kuanza kuzalisha baada ya upanzi.

Korir alisema wiki ya kwanza alivuna kilo 20, kiwango cha mavuno kikiendelea kuongezeka kila wiki kulingana na matunzo kwa njia ya maji na pia mbolea kuyastawisha na kunawirisha.

Anasema kufikia sasa anavuna zaidi ya kilo 240 kwa wiki. Kwa kuwa wateja wake ni wanunuzi wa kijumla, kilo moja haipungui Sh60 bei ya jumla. “Bei ya karakara hulingana na wakati, nyakati zingine huongezeka hadi Sh100 kwa kilo,” mkulima huyo anaelezea.

Kulingana na Daniel Mwenda, mtaalamu wa kilimo cha mwenda matunda, ekari iliyotunzwa kwa kuzingatia vigezo faafu si ajabu ikizalisha kilo 800 kila wiki.

Aligura kazi iliyomlipa mshahara wa Sh25, 000 kwa mwezi, kufanya kilimo cha karakara. Anaungama ukuzaji wa matunda haya ni faida tupu. PICHA/ SAMMY WAWERU

“Wakulima wanahimizwa kukumbatia mfumo wa kunyunyizia mimea na mashamba maji kwa mifereji. Kabla kuingilia kilimo cha matunda yoyote yale, hakikisha una chanzo cha maji ya kutosha,” Mwenda ambaye ni mwasisi wa shirika la kibinafsi Mwenda D Agroforestry Solutions, linalotoa huduma za kilimo cha matunda na miti anashauri.

Tayari mkulima Korir amepanua mradi wake kwa kuongeza ekari moja zaidi, akisema siku za usoni huenda shamba lao likapambwa kwa matunda ya karakara kwa sababu ya mapato yake kifedha. “Kilimo cha nafaka, mahindi, ngano na maharagwe, mazao huwa mara moja pekee kwa mwaka. Karakara mazao yake ni mfululizo ikiwa una kiini cha maji ya kutosha.

“Isitoshe, soko la nafaka North Rift ni kikwazo kwa sababu ya bei duni, ndio maana wakulima hulalamika kila wakati. Soko la karakara ni tayari, wateja hujia matunda shambani na hata hayapatikani kwa sababu wakulima wake ni wachache mno,” anafafanua mkulima huyo mchanga.

Ni kufuatia mapato ya kuridhisha ya karakara ambayo yalimchochea kugura ajira jijini, na kuendeleza kilimo cha matunda hayo kikamilifu.

Korir anashangaa ni kwa namna gani wakulima wengi wanaendelea kuwa mateka wa mimea ambayo soko lake ni mahangaiko tupu, ilhali kilimo cha karakara yeye hutabasamu akielekea benkini kuweka akiba ya mapato. “Ukulima wa karakara unaweza kukuondoa kutoka maisha ya uchochole uingie ligi ya wadosi chini ya muda mfupi,” anaelezea, akionekana kuridhishwa na jitihada zake katika kilimo hicho.

Kijana huyo anasema ni muda mfupi tu amejipa, hivi karibuni aingie kwenye orodha ya mamilionea wachanga nchini.

Akilinganisha mapato ya nafaka na karakara, anasema kilimo cha karakara kinaweza kukufanya mkwasi chini ya muda mfupi. PICHA/ SAMMY WAWERU

Cha kutia moyo, Korir anasema ukuzaji wa karakara hauna gharama ya juu ukilinganishwa na nafaka na mimea mingine. “Muhimu ni kuwa na maji ya kutosha,” anasema, akidokeza kwamba ana kisima.

Alianza kujizalishia miche, hatua ambayo anaisifia kumuondolea gharama ya kuinunua. “Mimi ndiye hujipandikizia mwenyewe na kuitunza,” aeleza mkulima huyo.

Kulingana naye, upanzi wa karakara hauhitaji mwalimu. Huandaa mashimo ya kipimo cha futi mbili urefu, na kipenyo cha kimo sawa na hicho.

Aidha, nafasi kati ya mashimo anasema huipa mita mbili hadi tatu, mistari ya mashimo nayo akipendekeza isipungue mita tano.

“Hupanda kwa mbolea ya ng’ombe au mbuzi,” aeleza mkulima huyo. Korir pia ni mfugaji, hivyo basi gharama ya mbolea kwake si hoja.

James Macharia mtaalamu wa kilimo anashauri: “Udongo wa juu uchanganywe na mbolea, mchanganyiko huo urejeshwe hadi kimo cha robo tatu ya shimo. Panda mche, kisha uendelee kuutunza kwa maji, mbolea na fatalaiza.”

Mdau huyo anasema kuwa robo iliyosalia, ni ya shughuli za kuzuia uvukuzi wa maji kwa kuweka nyasi za boji (mulching). Mbali na maji, matunzo mengine muhimu katika kufanikisha ukuzaji wa karakara ni kuweka mboleahai ya mifugo na pia fatalaiza kwenye shina la mkarakara ili kunawirisha mazao.

Kwa sababu ni matunda ya kutambaa, isitiri kwa vikingi vilivyounganishwa kwa nyaya katika kilele cha kila kikingi. Kati ya mwezi wa nne hadi wa saba baada ya upanzi, huanza kuchana maua na kutunda.

You can share this post!

Watoto 5 wapatikana wameuawa

Spika wa Migori apiga ripoti polisi baada ya kutishiwa...