• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 10:55 AM
Polisi hawahusiki na utekaji nyara wala mauaji – Mutyambai

Polisi hawahusiki na utekaji nyara wala mauaji – Mutyambai

MISHI GONGO NA WACHIRA MWANGI

INSPEKTA jenerali wa polisi Bw Hillary Mutyambai amewaonya Wakenya dhidi ya kuwahusisha maafisa wa polisi na visa vya utekaji nyara na mauaji yanayoendelea nchini. 

Bw Mutyambai alisema visa hivyo vinatekelezwa na majambazi wanaojifanya kuwa maafisa wa polisi.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika Hotelini Sarova Whitesands mjini Mombasa, Bw Mutyambai aliwaomba Wakenya kutaja majina ya maafisa wanaotekeleza uovu huo.

“Ikiwa unamjua afisa wa polisi anayetekeleza uovu huu, naomba uwasilishe jina lake kwetu, mkifanya hivi mutaniwezesha kutatua tashwishi hii,”akasema Bw Mutyambai.

Kati ya Wakenya milioni 47, haiwezekani kuwa mafisa wa polisi kunyooshewa vidole bila ushahidi wowote.

Kama ni kuwahukumu tunapaswa kuwa na ushahidi ambao utatuwezesha kuwachukulia hatua,”akasema.

Maeneo ya Pwani na kaskazini mashariki mwa Kenya yamekuwa yakishuhudia visa vya watu kupotezwa na kuuawa bila kujua anayetekeleza maovu hayo.

Mara nyingi wanaouawa huhusishwa na tuhuma kuwa wanachama wa makundi ya kigaidi.

Bw Mutyambai alisema maafisa wengi wa polisi ni wachapa kazi, akiongezea kuwa yuko tayari kukabiliana na wachache ambao ni watovu wa nidhamu.

“Tunapaswa kuangalia asilimia 96.5 ambao wanafanya kazi nzuri.Tusiwavunje moyo maafisa wanaofanya kazi wakati nyinyi mmelala,” akasema.

“Iwapo kuna mtu ambaye anatekeleza uwovu huo basi tunawaomba mulete jina lake. Kuwahukumu maafisa wa polisi bila ushahidi si haki,” akasema.

Aidha Bw Mutyambai alisema maafisa wa polisi wamefanya kazi nzuri katika kukabili uhalifu katika maeneo ya Kisauni, ambalo limekuwa likihangaishwa na magenge ya Wakali kwanza na wakali wao,Al shabaab na walanguzi wa madawa ya kulevya.

Inspekta huyo alisema anafanya kazi kwa karibu na mkurugenzi wa mashtaka ya umma kuhakikisha wanawaadhibu wahalifu.

Juma lililopita katika maadhimisho ya kuwakumbuka waliyopotezwa na kuuwa makundi ya kutetea haki za kibinaadamu yaliisukuma serikali kuunda jopo litakalo chunguza mauwaji yanayoendelea nchini na kuwachukulia hatua wahusika.

Kaunti ya Kwale ilisema imeandikisha visa 28 vya watu waliyopotezwa na kuuwawa kati yam waka 2019 na 2020.

Huku Mombasa wakisema kuwa wameandikisha visa 22.Aidha makundi hayo pia yaliomba familia za waliyopotezwa kulipwa fidia.

You can share this post!

BBI: Vigogo sasa waelekeza zana zao makanisani

Mabwanyenye wa Ukambani mbioni kupimana ubabe