Wavuvi 6,000 wapewa vitambulisho vya baharini Lamu
NA KALUME KAZUNGU
ZAIDI ya wavuvi 6000 wa Lamu wanalengwa katika zoezi linaloendelea la kusajili wavuvi hao kwa njia ya kielektroniki ili wakabidhiwe vitambulisho maalum.
Zoezi hilo linalenga kuimarisha usalama wa wavuvi kila mara wanapokuwa baharini wakitekeleza shughuli zao.
Wavuvi wa Lamu wamekuwa wakikumbwa na wakati mgumu mikononi mwa walinda usalama hasa tangu serikali ilipopiga marufuku uvuvi wa usiku eneo hilo mnamo 2011 kufuatia utovu wa usalama uliokuwa ukichangiwa na magaidi wa Al-Shabaab.
Marufuku hiyo aidha iliondolewa mnamo 2019 baada ya waziri wa usalama wa ndani, Fred Matiangí kuzuru Lamu na kuamuru wavuviu wote wasajiliwe kwa njia ya kielektroniki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, alisema kila mvuvi eneo hilo atakabidhiwe kitambulisho chake maalum, maarufu ‘Mvuvi Card,’atakachokuwa akibeba kila mara anapokuwa baharini.
Kitambulishoi hicho kitajumuisha jina la mvuvi, nambari yake ya kitambulisho cha kitaifa na kikundi cha wavuvi (BMU) ambacho mvuvi husika ni mwanachama wake.
Kitambulisho hicho pia kitawezesha maafisa wa usalama kutambua eneo ambako mvuvi huyo atakuwa akivua baharini.
Bw Macharia alisifu mpango huo, akisisitiza kuwa utasaidia pakubwa kudhibiti usalama wa baharini kote Lamu.
Kulingana na Bw Macharia, baadhi ya magaidi wamekuwa wakitumia mbinu ya bahari, ambapo hujifanya kuwa wavuvi huku wakiendeleza ajenda zao za mashambulizi.
Alisema vitambulisho hivyo vitasaidia kuwanasa kwa urahisi wahalifu baharini.
“Serikali imeanzisha shughuli ya kuwasajili wavuvi ili kuwapa vitambulisho maalum. Tunalenga wavuvi wapatao 6000 kote Lamu. Kadi husika itarahisisha utendakazi wa maafisa wa usalama wanaoshika doria baharini na pia kudhibiti usalama wa wavuvi. Itatuwezesha kuwatambua wavuvi halisi na magaidi baharini,” akasema Bw Macharia.
Miongoni mwa mashirika yaliyosaidia katika ufadhili na uzinduzi wa mpango huo wa usalama wa wavuvi wa Lamu ni Search for Common Grounds, Kiunga Youth Bunge Initiative (KYBI) na Muungano wa Bara Ulaya (EU).
Katika mahojiano na wanahabari muda mfupi baada ya shughuli ya kuwasdajili wavuvi wa Lamu kuzinduliwa, Meneja Mkuu wa Search for Common Grounds, Mohamed Mwachausa aliwasisitizia wavuvi kujitokeza vilivyo ili wasajiliwe kupata kadi hiyo ya usalama baharini.
“Hii ni fursa ya wavuvu kujitokeza kikamilifu ili wasajhiliwe kupata vitambulisho hivyo maalum ili wafanye shugh8uli zao kila siku bila kutatizwa na walinda usalama,” akasema Bw Mwachausa.
Kwa upande wake, Afisa wa Idara ya Uvuvi, Kaunti ya Lamu, Bw Simon Komu alisifu mpango huo, akisisitiza kuwa utaongeza pato la samaki kote Lamu kwa hadi asilimia 75.