Habari Mseto

Mudavadi aitaka seneti itanzue mvutano kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha

September 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

ERIC MATARA na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa chama cha ANC Musalia Mudavadi amewataka maseneta wakubaliane na kutanzua mvutano kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha kwa kaunti ili kaunti zisambaziwe fedha.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bw Mudavadi alitoa wito kwa maseneta hao kusuluhisha mvutano huo Jumanne seneti itakaporelea vikao baada ya likizo ya mwezi mmoja.

“Mvutano kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha unaweza kuathiri nchi pakubwa. Serikali sasa zinapitia hali ngumu baada ya kucheleweshwa kwa usambazaji wa fedha kutoka Hazina ya Kitaifa. Magavana wanalalamika kwa sababu shughuli zimekwama na wafanyakazi hawajalipwa mishahara kwa miezi miwili,” akaambia Taifa Leo.

Kiongozi huyo wa ANC aliwataka maseneta kuweka kando tofauti zao za kibinafsi na kisiasa na watatue suala hilo.

Tayari, Baraza la Magavana (CoG) , kupitia mwenyekiti wake Wycliffe Oparanya, limetisha kusitisha shughuli katika kaunti zote 47 ikiwa mvutano kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha hautakuwa umetatuliwa kufikia Septemba 17.

Wiki jana Bw Oparanya ambaye ni Gavana wa Kaunti ya Kakamega alisema mvutano huo ukiendelea watawaamuru wafanyakazi wasalie nyumbani hadi suluhu lipatikane.

Magavana pia wametisha kuanzisha mchakato wa kufutiliwa mbali kwa bunge la Seneti ikiwa maseneta wataendelea kuvutana kuhusu suala hilo.

Kamati ya muda ya wanachama 12 iliyobuniwa kusaka mapatano kuhusu suala hilo, baada ya maseneta kushindwa kuelewana katika mara yake 11, wiki jana ilielezea matumaini ya kupatikana kwa muafaka.

Lakini duru zimeambia Taifa Leo kwamba kamati hiyo iliwasilisha ripoti mbili kwa uongozi wa Seneti; ishara ya ukosefu wa maelewano miongoni mwa wanachama wake.

Baadhi ya wanachama wake wangali wanasisitiza kuwa Sh316.5 bilioni zilizotengewa kaunti sharti zigawanywe kwa msingi wa idadi ya watu katika kaunti huku wenzao wakipendelea kigezo cha ukubwa wa kaunti.