• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
Maandamano Thika Road kufuatia mauaji ya mkazi Githurai

Maandamano Thika Road kufuatia mauaji ya mkazi Githurai

Na SAMMY WAWERU

SHUGHULI za usafiri na uchukuzi Thika Superhighway Alhamisi zimetatizika kwa muda kufuatia maandamano ya wakazi wakilalamikia mauaji ya kikatili ya mmoja wao.

Inadaiwa yalitekelezwa na maafisa wa polisi.

Waandamanaji hao walifunga barabara eneo la Githurai, wakidai mmoja wa wakazi Githurai 44 aliuawa kinyama katika hali isiyoeleweka mikononi mwa polisi.

Aidha, walionyesha ghadhabu zao kwa kurusha miamba ya mawe barabarani na kuteketeza magurudumu kwa moto. Maandamano hayo, kulingana na tuliozungumza nao yalianza mwendo wa saa tatu asubuhi.

Maafisa wa polisi walilazimika kutumia gesi ya vitoa machozi na maji, kutawanya waandamanaji ili kufungua barabara.

“Tunataka haki, na kuelezwa bayana kwa nini mmoja wetu akauawa mikononi mwa polisi wanaopaswa kutulinda,” akasema mmoja wa waandamaji.

Inadaiwa kwamba mkazi huyo alikamatwa na maafisa wa polisi (siku ambayo haijafahamika wala maelezo zaidi kumhusu), kisha baadaye akapatikana ameuawa.

Juhudi za kujaribu kuzungumza na maafisa kadhaa wa polisi hazikufua dafu, wakisema “hata nasi hatujui kinachoendelea, tumeitika wito kufungua barabara baada ya waandamanaji kuifunga”. Walisema hawana idhini kuzungumza na waandishi wa habari.

Mmoja wa Afisa msimamizi wa Polisi Kaunti Ndogo ya Ruiru na aliyeomba kubana jina lake, kwa njia ya simu hata hivyo alisema alifahamishwa kuhusu maandamano hayo na kwamba alipata fununu yalisababishwa na mauaji ya mkazi mikononi mwa maafisa wa polisi. “Mkuu wa Polisi Kituo cha Kasarani atawaambia sababu halisi za maandamano hayo,” akaambia Taifa Leo.

Huku hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda, maafisa wa polisi kukabiliana na ghasia (GSU) wametumwa kupiga doria.

Maafisa wa polisi wanaendelea kunyooshewa kidole cha lawama kufuatia ongezeko la mauaji ya raia mikononi mwao, hasa kipindi hiki cha corona.

You can share this post!

Uhuru azima pensheni ya wabunge wa zamani

DPP aamuru Ali Korane atiwe mbaroni kwa tuhuma za ufisadi