• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Kongamano la kujadili ufunguzi wa shule kufanyika Nairobi Septemba 14

Kongamano la kujadili ufunguzi wa shule kufanyika Nairobi Septemba 14

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Elimu George Magoha ameitisha kongamano la wadau katika sekta ya elimu mnamo Septemba 14, 2020, kujadili taratibu za kufunguliwa kwa shule na vyuo.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Septemba 11, 2020, Profesa Magoha amewaalika wadau hao katika kongamano hilo ambalo litafanyika katika Taasisi ya Kuandaa Mitaala Nchini (KICD), Nairobi.

Katika mkutano huo ambao utaanza saa mbili asubuhi, washiriki watahitaji kutoa maoni yao kuhusu mwongozo utakaozingatiwa kurejelewa kwa masomo baada ya visa vya Covid-19 kupungua katika kiwango hitajika kisicholeta sana wasiwasi.

“Wadau wote katika sekta ya elimu wanaalikwa katika kongamano ili watoe maoni na mapendekezo yao kuhusu mwelekeo utakaofuatwa kurejelewa kwa masomo baada ya kupungua maambukizi ya corona,” ikasema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Prof Magoha.

Mnamo Julai 2020 Waziri huyu wa Elimu alitangaza kuwa shule zingesalia kufungwa hadi Januari 2021 kufuatia kupanda kwa visa vya maambukizi ya virusi vya corona.

Lakini juzi alidokeza kuwa huenda shule zitafunguliwa kabla ya Januari 2021 ikiwa kiwango cha maambukizi kitashuka hadi chini ya asilimia tano kwa wiki mbili mfululizo.

Kwa muda mrefu sasa visa hivyo havijazidi 200 kwa siku, hali ambayo imeongeza matumaini kwamba huenda serikali ikalegeza zaidi masharti yaliyowekwa kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.

Mkutano wa Ijumaa

Jopokazi lililobuniwa kuandaa mwongozo wa ufunguzi wa shule lilikutana Ijumaa chini ya uongozi wa Prof Magoha kujadili matayarisho ya shule kwa kuelekea ufunguzi wa shule.

Tayari wanasiasa, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta, wameanza kuhutubia mikutano ya hadhara kinyume cha masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya.

Wengine ni Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga, mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi na wabunge kadhaa akiwemo Oscar Sudi (Kapseret).

Mnamo Agosti 25, 2020, mzazi mmoja aliwasilisha kesi mahakamani kumshurutisha waziri Magoha kufungua shule na taasisi zingine za masomo.

Bw Joseph Aura anataka mahakama itoe agizo la kuilazimisha serikali itoe mwelekeo kuhusu ni lini shule zitafunguliwa.

Akiwakilishwa na wakili Harrison Kinyanjui, Bw Aura alisema shule kusalia kufungwa kwa kipindi kirefu kuanzia Machi, bila mashauriano na wazazi, ni kinyume cha Sheria ya Elimu ya Msingi.

Vile vile, alimkosoa Prof Magoha kwa kugeuza baadhi ya shule kuwa vituo vya karantini kutumiwa na watu wanaoshukiwa kuambukizwa Covid-19.

“Hii ni kinyume cha kipengee cha 32 cha Sheria ya Afya,” Bw Aura alisema katika stakabadhi ya kesi.

Vile vile, Bw Aura anataka serikali iwalipe fidia wanafunzi ambao wameathirika kisaikolojia kutokana na kufungwa kwa shule kwa kipindi kirefu.

You can share this post!

NCIC yapendekeza wanasiasa wachochezi wazimwe uwaniaji

Kaunti kusubiri idhini ya bunge ili zipate...