Habari Mseto

Kaunti kusubiri idhini ya bunge ili zipate 'advansi' – Kihara

September 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MWANASHERIA Mkuu Kihara Kariuki amesema serikali za kaunti zinaweza kusambaziwa asilimia 50 ya fedha za mgao zilizofaa kupata, endapo Bunge la Kitaifa litaidhinisha hatua hiyo.

Hii itatoa afueni kubwa kwa serikali 47 za kaunti ambazo zinakabiliwa na ukosefu wa fedha baada ya maseneta kuvutana kwa muda mrefu na kushindwa kupitisha mfumo mpya wa ugavi wa fedha kwa kaunti.

Maseneta wamefanya vikao tisa kujadili suala hilo lakini hawajaelewana kuhusu suala hilo. Kamati ya maseneta 12 ya kusaka mwafaka kuhusu suala hilo pia haijafua dafu baada ya kuibuka na mapendekezo mawili kinzani.

“Fedha zinaweza kutolewa kutoka Hazina ya Jumla (Consolidated Fund) kufuatia idhini ya bunge la kitaifa. Fedha hizo zitasambazwa kwa kuzingatia Sheria ya Ugavi wa Fedha Baina ya Kaunti (CARA) ya mwaka wa kifedha uliopita. Hii ni kufungamana na ushauri uliotolewa na Mahakama ya Juu kwamba ikiwa usambazaji wa fedha utafanywa kwa kuzingatia sheria ya CARA ya mwaka wa kifedha uliotangulia, sharti bunge la kitaifa liidhinishe kutolewa kwa fedha hizo kutoka Hazina ya Jumla,” Bw Kihara akasema kwenye taarifa Ijumaa, Septemba 11, 2020.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu alisema afisi yake haiwezi kuruhusu fedha hizo (asilimia 50) zitolewe kwa misingi ya Sheria ya Ugavi wa Fedha (DORA) iliyopitishwa mwaka huu, 2020.

Hata hivyo, sheria inaruhusu fedha kusambazwa kwa matumizi ya Serikali Kuu kabla ya kupitishwa kwa Sheria ya Ugavi wa Fedha kwa Idara Mbalimbali (Appropriation Act).

“Msimamo wetu ni kuwa sheria ya kuwezesha usambazaji wa fedha kwa serikali za kaunti ni CARA pekee,” Bw Kihara akasema.

Kwa hivyo, Mwanasheria huyo Mkuu ameishauri Hazina ya Kitaifa kutumia sheria ya CARA ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020, wakati huu ambapo mfumo wa ugavi haujapitishwa.

Ni baada ya kupitishwa kwa mfumo mpya ya ugavi wa fedha kwa kaunti ambapo Seneti inaweza kupitisha Sheria ya Ugavi wa Fedha Baina ya Kaunti (CARA) ya 2020. Hii ndiyo sheria inayofaa kutumiwa kugawa fedha kwa kaunti katika mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021.

Bw Kihara alitoa ushauri huu kufuatia barua aliyoandikiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya akitaka ushauri wake kuhusu iwapo serikali za kaunti zinaweza kupewa asilimia 50 ya mgao wa fedha.

CoG imekuwa ikiishinikiza Hazina ya Kitaifa kutoa fedha hizo haraka ili kaunti ziweze kugharimia shughuli za dharura katika ulipaji mishahara ya wafanyakazi.

Baadhi ya Kaunti, kama vile Kisumu, zimekopa fedha za kulipa mishahara kutoka kwa benki za humu nchini.

Wiki jana Bunge la Kaunti ya Kisumu liliidhinisha ombi la Gavana Anyang’ Nyong’o la kutaka kukopa Sh400 milioni kutoka Benki ya KCB, ilipe wafanyakazi.

Bw Oparanya pia alisema kaunti zinahitaji fedha za kugharimia bima ya afya kwa wahudumu wa afya wakati huu wa janga la Covid-19.

“Wito wetu kwa Seneti kwamba ikamilishe suala la mfumo wa ugavi wa fedha haujazingatiwa. Kamati ya watu 12 iliyobuniwa kusaka muafaka kuhusu suala hilo pia haijafaulu. Hali hii sasa inaathiri shughuli za utoaji hudumu katika Serikali za Kaunti na kuchelewesha mishahara ya wafanyakazi,” Oparanya ambaye ni Gavana wa Kakamega alisema kwenye taarifa wiki jana.

Alisema magavana watalazimika kusitisha shughuli katika kaunti kufikia Alhamisi, Septemba 17, 2020, ikiwa kaunti hazitakuwa zimepokea fedha.