• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Kebs yaharibu kwa kuteketeza bidhaa ambazo muda wa matumizi ulipita

Kebs yaharibu kwa kuteketeza bidhaa ambazo muda wa matumizi ulipita

Na MISHI GONGO

SHIRIKA la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (Kebs) limeteketeza tani 64 za mchele na spaghetti, bidhaa hizi zikiwa za thamani ya Sh10 milioni mjini Mombasa katika juhudi zake za kuendelea kudhibiti matumizi ya bidhaa ghushi na zilizoharibika nchini.

Kulingana na mkuu wa shirika hilo katika eneo la Pwani Bw Cirus Wambani shehena hiyo haikuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Alisema japo shehena hiyo iliingizwa nchini kihalali ilichukuwa muda mwingi katika maghala hadi kuharibika.

Akizungumza wakati shughuli ya uteketezaji ikiendelea katika eneo la Kibarani Bw Wambani alisema shehena hiyo ilikuwa tani 58 za spaghetti za Ziana na mchele tani sita zilizokuwa zimewekwa katika maghala mbalimbali eneo la Shimanzi.

Mkuu huyo alisema wamekaza kamba katika kusaka bidhaa ambazo hazifai kuliwa na binadamu.

“Tumekaza kamba kuhakikisha kuwa wakazi wanatumia bidhaa bora. Pia tunataka kuhakikisha kuwa bidhaa zilizopitisha muda wa ubora haziingii sokoni,” akasema mkuu huyo.

Kilingana na afisa wa uchunguzi wa makosa ya jinai mjini Mombasa (CID) Bw Washington Njiru shehena hiyo iliingia nchini mwaka 2017 na muda wa kuharibika ulikuwa Julai 2019.

Alisema walinasa shehena hiyo ambayo waliamini kuwa ingepakiwa upya na kusambazwa sokoni kwa ushirikiano wa mafisadi mbalimbali katika serikali.

“Bidhaa zilipoingia nchini zilikuwa salama na zilipitia vigezo vyote kuthibitisha ubora wake kabla ya kuingia nchini,lakini waliyoleta shehena hiyo walichelewa kuisambaza sokoni,” akasema Bw Njiru.

Mshirikishi wa usalama katika eneo la Pwani Bw John Elungata aliyesimamia kuchomwa huko aliwaomba Wakenya kushirikiana na maafisa wa serikali kuhakikisha kuwa bidhaa mbovu haziingii nchini.

“Kuna watu wanataka kujitajirisha kwa kuwaweka wakazi katika hatari za kiafya. Tunawaomba Wakenya kutoruhusu wakora kujitajirisha,” akasema.

Alisema kuwa kumekuwa na visa vya watu kufunga bidhaa zilizoharibika na kuzisambaza.aliwaomba maafisa katika mamlaka ya bandari kuwa makini katika kuchunguza bidhaa zinazoingizwa nchini.

You can share this post!

Wakenya bado mateka kisiasa

Kocha Nuno Espirito kurefusha mkataba wake kambini mwa...