Walimu walalamikia mwongozo mpya wa kuwapandisha vyeo
Na FAITH NYAMAI
WALIMU wa shule za msingi kote nchini sasa wametoa wito kwa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) isitumie mwongozo mpya ya kuwapandisha vyeo, wakisema itawafungia wengi wao nje licha ya kuhudumu kwenye taaluma hiyo kwa miaka mingi.
Wengi wao wanahoji kwamba itawachukua zaidi ya miaka tisa wapandishwe cheo ndipo watumikie nyadhifa za naibu wa mwalimu mkuu au mwalimu mkuu.
Walimu ambao wako kwenye kiwango cha mshahara wa daraja la T, gredi ya 7 wanadai kwamba wamesalia katika kiwango hicho kwa muda wa zaidi ya miaka 15 na hawawezi kupandishwa vyeo kuwa walimu wakuu au manaibu wa walimu wakuu licha ya uzoefu wa miaka mingi kazini.
Baadhi ya walimu waliozungumza na Taifa Jumapili, walidai kuwa wenzao kwenye kiwango cha mshahara wa T, gredi ya 8, wamepandishwa vyeo hadi kuwa manaibu walimu wakuu baada ya kupandishwa cheo awali hadi kuwa mwalimu mwandaamizi mnamo 2017.
“Wakati ambapo nafasi za manaibu walimu wakuu zilitangazwa, maombi ya walimu waandamizi wa gredi ya pili yalikataliwa na TSC wakidaiwa kuwa hawakufuzu,” akasema mwalimu ambaye hakutaka atajwe jina.
“Wengi wetu walikuwa wamehudumu kama walimu waandamizi kwa muda wa miaka mitatu kabla ya mwongozo mpya wa kupandisha walimu vyeo maarufu kama CPG kuanza kutumika. Hiyo ndiyo maana tumesalia katika kiwango kimoja cha mshahara kwa miaka sita,” akaongeza.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu (KNUT) Hesborn Otieno, jana alisema CPG imesababisha mwanya mkubwa katika taaluma ya ualimu na kuwanyima wengi waliokuwa wakitarajia wapandishwe vyeo kazini.
“Mwongozo wa CPG haukujadiliwa na TSC ilianza kuutekeleza bila kupokea maoni ya Knut. Hiyo ndiyo sababu kuu walimu hawawezi kupandishwa vyeo ili waongezewe mishahara,’’ akasema Bw Otieno.
Afisa huyo aliongeza kwamba utekelezaji wa CPG na makubaliano ya CBA pia hayakujumuisha maslahi ya walimu wanaosimamia madarasa mbalimbali.
“Wangekubali tujadili mwongozo huo kabla utekelezwe,” akaongeza.
Muda
Mkurugenzi wa mawasiliano kwenye TSC Beatrice Wababu hata hivyo alisema alihitaji muda zaidi wa mashauriano kabla ya kutoa kauli yake kuhusu mwongozo huo tata wa kuwapandisha walimu vyeo.
“Niruhusu nifanye mashauriano kisha nitarejea kwako,” akasema.
Mnamo 2018, TSC iliibuka na miongozo miwili ya kuwapandisha vyeo walimu wandamizi. CPG ilianza kutumia na kuchukua sehemu ya kigezo cha kuhudumu kwenye taaluma ya ualimu ambacho kilizingatia sana miaka ya kufundishia na kiwango cha masomo.
Kukumbatiwa kwa CPG kulimaanisha kwamba walimu waandamizi sasa watalazimika wasubiri hadi 2023 ili watume ombi ndipo wapandishwe cheo kuwa manaibu walimu wakuu.
“Walimu waandamizi katika viwango viwili vya kazi na mishahara wanafanya kazi sawa za usimamizi wa shule na wanafuzu kuwa walimu wakuu. Mwongozo huu wa CPG unapendelea upande moja tu,” akasema mwalimu mwengine.
Viongozi wa Knut na wanachama wa TSC wanatarajiwa wafike bungeni mnamo Jumatano kuhusu suala hilo tata la kuwapandisha walimu vyeo.