Kesi ya Jaji Mwilu yajikokota Maraga akikaribia kustaafu
WANJOHI GITHAE na IBRAHIM ORUKO
TUME ya Huduma za Mahakama (JSC) bado haijasikia kesi nne dhidi ya Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu, miaka miwili baada ya kesi ya kwanza kuwasilishwa kortini huku muda wa kustaafu kwa Jaji Mkuu David Maraga ukiwa umesalia miezi mitatu pekee utimie.
Bw Maraga anatarajiwa atastaafu rasmi Januari mwakani lakini ataanza likizo ya lazima mnamo Disemba 15 hali ambayo itaiacha idara ya mahakama mikononi mwa Bi Mwili anayekabiliwa na kesi nne kortini.
Jaji Mwilu kikatiba atakuwa kaimu Jaji Mkuu kabla mwengine kuteuliwa rasmi ikizingatiwa pia mchakato wa kumteua mrithi wa Bw Maraga utachukua muda kisheria.
Kesi ya kwanza dhidi ya Bi Mwilu iliwasilishwa mnamo Oktoba 2018, na Mogire Mogaka huku nyingine tatu zikifikishwa kortini Juni 2019 na afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa ushirikiano Idara ya uchunguzi wa makosa ya uhalifu (DCI) huku Wakenya Alexandre Mugane na Peter Kirika pia wakiwasilisha kesi zao kila moja.
UAMUZI
Hata hivyo, mawakili wa Bi Mwilu wamekuwa wakitumia njia zote za kisheria kuzuia kesi hizo kusikizwa mbele ya JSC hali ambayo imechelewesha uamuzi kutolewa dhidi ya Jaji Mwilu.
Mnamo Agosti 17, 2020, Jaji Weldon Korir alitoa amri inayozuia JSC kusikiza malalamishi dhidi ya Jaji Mwilu hadi kesi zote zilizowasilishwa mahakamani zinazomhusisha zisikizwe na ziamuliwe.
Naibu Jaji Mkuu pia alipinga uamuzi wa JSC wa kutupilia mbali ombi lake la kuwataka mwanasheria mkuu Kihara Kariuki na mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Macharia Njeru wajiondoe kwenye jopo la kusikiza malalamishi dhidi yake katika tume hiyo.
Isitoshe katika kesi zake zilizoko mahakama kuu, Jaji Mwilu anadai zingine zilizowasilishwa DPP, DCI, Mabw Mugane, Kirika na Mogaka zinahusiana na kesi nyingine iliyoko katika mahakama ya rufaa ambayo vilevile haijaamuliwa.
Hata hivyo, Msajili wa mahakama kuu na katibu wa JSC Anne Amadi alipinga hoja zote zilizoibuliwa na Jaji Mwilu akitaka Bw Kariuki na Bw Njeru wajiondoe kusikiza malalamishi yake kwenye tume hiyo.
“JSC inatambua kwamba mwenyekiti wa JSC ambaye ni Jaji Mkuu atastaafu Januari 2021 na mrithi wake ni Jaji Mwilu ambaye anakabiliwa na malalamishi na kesi. Kutakuwa na pengo kortini ikizingatiwa Naibu Jaji Mkuu pia ni mwanachama wa JSC na husikiza malalamishi dhidi ya majaji mengine. Tunaomba kesi zote nne dhidi ya Naibu Jaji Mkuu zishughulikiwe haraka tena kwa dharura,” Bi Amadi akaeleza mahakama wiki hii.
Bi Mwilu alikamatwa mnamo Agosti 28,2018 na kufikishwa kortini siku hiyo lakini hakujibu mashataka kuhusu kesi za ufisadi zinazomkabili.