• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
Huyu Mutua ni twiga, amejitokeza ChapChap!

Huyu Mutua ni twiga, amejitokeza ChapChap!

Na BENSON MATHEKA

KUJITOSA rasmi kwa Gavana wa Machakos Alfred Mutua katika kinyang’anyiro cha urais kwenye uchaguzi mkuu ujao ni mbinu yake ya kuhakikisha nyota yake ya kisiasa itaendelea kunawiri hata baada ya kukamilisha kipindi chake cha pili cha ugavana.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba kuzindua kampeni yake miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu na wakati ambapo kuna pendekezo la kubadilisha Katiba ni mbinu ya kujiandaa kunufaika kutokana na miungano mipya ya kisiasa iinayonukia uchaguzi mkuu ujao unapokaribia.

Wiki jana, Dkt Mutua alitangaza kuwa atakuwa kwenye debe katika uchaguzi wa urais ujao ili kuleta mwamko mpya wa utawala nchini ambao utahakikisha upatikanaji wa haraka wa maendeleo.

Alikuwa gavana wa kwanza anayehudumu kipindi cha pili kuzindua rasmi kampeni ya kugombea urais. Magavana wenzake wanaomezea mate urais ni Kivutha Kibwana wa Makueni, Wycliffe Oparanya wa Kakamega na Hassan Joho wa Mombasa.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba ikizingatiwa kuwa Dkt Mutua ni mtaalamu wa masuala ya mawasiliano na kwamba kuna mabadiliko ya kisiasa yanayotarajiwa nchini, hatua yake inaashiria anajipanga ili kujihakikishia nafasi katika siasa za kitaifa.

“Ni mbinu ya kujipanga ili kuhakikisha kuwa, nyota yake ya kisiasa itaendelea kunawiri baada ya kumaliza kipindi chake cha pili kama gavana. Anataka kucheza ligi ya siasa za kitaifa na anafahamu kufanya hivyo kunahitaji kujitangaza,” asema mdadisi wa siasa Bonface Kiilu.

Kwa mujibu wa mdadisi huyo, hatua ya Dkt Mutua inanuiwa kujiweka katika ngazi moja na viongozi wengine wanaoshiriki siasa za kitaifa eneo la Ukambani kama kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Charity Ngilu wa chama cha Narc na Kivutha Kibwana ambao wamejijengea sifa kitaifa kwa miaka mingi.Bw Musyoka na Bw Kibwana pia wanamezea mate urais.

“Ingawa Mutua alihudumu kama msemaji wa serikali kwa miaka saba, tajriba yake katika siasa haiwezi kufananishwa na ya Bw Musyoka ambaye amekuwa mbunge na waziri kwa miaka mingi na makamu wa rais.

Kibwana naye amewahi kuwa mbunge, mhadhiri, waziri na ni mtaalamu wa masuala ya kikatiba ilhali Bi Ngilu alikuwa mbunge, waziri na mgombea urais. Kwa hivyo, tunayoshuhudia ni mbinu za kujikweza aweze kufikia kiwango chao,” asema Bw Kiilu.

Mbinu hii, anaeleza, pia inanuiwa kumweka kifua mbele katika vita vya ubabe wa kisiasa eneo la Ukambani. Wadadisi wanasema Dkt Mutua anafahamu kuwa iwapo Katiba itafanyiwa mabadiliko na nafasi zaidi za uongozi kubuniwa, ni wanasiasa wanaoshiriki siasa za kitaifa pekee watakaonufaika na hatua ya kuzindua rasmi kampeni yake kunamweka katika nafasi nzuri.

Bw Jorum Mumo, mchanganuzi wa siasa anasema kwamba Dkt Mutua ni mwanasiasa mweledi ambaye hawezi kupuuzwa katika siasa za Kenya.

“Ninaamini miungano ya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 au baada ya uchaguzi huo itakapobuniwa, Dkt Mutua atakuwa katika siasa za kitaifa. Alidhihirisha hayo chama chake cha Maendeleo Chap Chap kilipopata wawaniaji kote nchini katika uchaguzi mkuu wa 2017 ingawa kilikuwa kichanga,” alisema.

Bw Mumo asema ni miungano ya kisiasa itakayobuniwa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 itakayoamua iwapo jina la Mutua litakuwa debeni.

“Kuna wanasiasa wengi ambao huwa wanatangaza na kuzindua azma zao za urais kwa lengo la kuwinda washirika wa kubuni miungano. Ikizingatiwa wakati ambao Dkt Mutua alizindua azma yake, nashawishika hili ndilo analolenga,” anafafanua na kuongeza kuwa demokrasia ya Kenya imethibitisha kuwa ni miungano ya kisiasa inayoshinda uchaguzi wa urais.

Ingawa Dkt Mutua alisema kwamba anategemea washirika wake nchini na ng’ambo kufadhili kampeni zake za urais, wadadisi wanatilia shaka uwezo wake wa kushindana na vigogo wa kisiasa kama Raila Odinga wa chama cha ODM na Gideon Moi wa Kanu miongoni mwa wengine.

Hata hivyo, Dkt Mutua anasema lengo lake ni kurejesha Kenya katika njia yake ya ustawi iliyovurugwa na utawala mbaya, ufisadi na kupuuza vijana.

“Kenya inahitaji kiongozi kijana, mbunifu, mkakamavu na mkomavu. Niko tayari kuipanga Kenya vyema iwe nchi yenye haki na ya watu tajiri walio na furaha,” Dkt Mutua alisema.

Japo anasema viongozi waliotangulia walifanya mengi, anaamini kuwa wakati umefika wa kuleta maono mapya kupitia kiongozi wa vitendo.

“Tumechoka na mipango ya serikali ambayo haitekelezwi,” asema. Bw Mumo anasema hatua ya Dkt Mutua inafungua ukurasa mpya wa vita vya kisiasa kati yake na Bw Musyoka eneo la Ukambani.

You can share this post!

Azma ya urais ya Wa Iria yachemsha mbio za urithi Mlima...

Ruto hajakomaa kisiasa, asubiri 2027 – Atwoli