• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Ruto hajakomaa kisiasa, asubiri 2027 – Atwoli

Ruto hajakomaa kisiasa, asubiri 2027 – Atwoli

JUMA NAMLOLA na PATRICK LANG’AT

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu), Bw Francis Atwoli amemtaka Naibu Rais William Ruto asubiri mwaka 2027, kwa kuwa hajakomaa kuongoza nchi.

Bw Atwoli ambaye ni mtu wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa chama cha ODM, Raila Odinga, alishangaa ni kwa nini Dkt Ruto anajipiga kifua ilhali muda wake wa kuongoza haujafika.

“Yeye (Ruto) labda ajaribu mwaka 2027. Huenda akawa na nafasi. Sasa hivi, hajakomaa kututawala mwaka 2022. Anajipiga kifua bure. Anapaswa kujifunza kutoka kwa Mzee Daniel Moi na kuwa mnyenyekevu,” akasema.

Akihutubia wanahabari nyumbani kwake Ildamat, Kaunti ya Kajiado, Bw Atwoli alifanya mzaha kuwa hata ndege walio shambaani mwake wanaamini hivyo.

“Wakati mwingine najiuliza usiku, Ruto kweli anaweza kuwa Rais mwaka 2022? Jibu kila mara huwa ni ‘La’. Hata ndege walio hapa katika boma langu wanajua kwamba yeye hatakuwa Rais,” akasema Bw Atwoli.

Kauli yake ilionekana kutilia nguvu msimamo wa Bw Odinga akiwa mjini Mombasa kwamba hajachoka kuwania urais.Mojawapo ya sababu za wafuasi wa Dkt Ruto kutaka urais ni kwamba Bw Odinga amezeeka baada ya kuwania urais zaidi ya mara tatu.

“Tutajenga madaraja tuingia Canaan. Nataka Wakenya wajue kwamba sijachoka. Msidanganywe na wale wanaokuja na pesa kugawa makanisani au misibani,” akasema Bw Odinga, akionekana kumlenga Naibu Rais.

Jana Dkt Ruto alisema hatishwi na ‘kelele za chura’ kwa kuwa ni wananchi watakaokuwa na kauli ya mwisho kwenye suala hilo.

“Msitishwe wala kushinikizwa kuacha kuunga mkono azma hii. Hao wanaojiita ‘Deep State’ na ‘System’ ni kama kibofu chenye upepo. Ni mkusanyiko wa wahalifu,” akadai alipohutubu baada ya maombi katika makanisa ya Free Pentecostal Baraka Church na Kitengela Methodist Church Kaunti ya Kajiado.

Akiandamana na zaidi ya wabunge 20 wanaomuunga mkono, Dkt Ruto aliwahimiza wananchi wasikubali wanasiasa wanaotaka kuirejesha nchi katika siasa zilizopitwa na wakati.

“Tumepita enzi za watu kufanya siasa za ukabila na chuki. Siasa zetu ni za maendeleo kwa lengo la kuibadili nchi yetu,” akasema Dkt Ruto.

Hata hivyo, kauli yake ilionekana kinyume na hali ilivyo, ambapo wanasiasa wanaomuunga mkono wamekuwa midomoni mwa Wakenya wiki nzima iliyopita, kwa kutoa matamshi yanayochukuliwa kuwa ya kikabila na yanayoweza kuzua ghasia.

Mbunge wa Emurua Dikirr, Bw Johanna Ng’eno Alhamisi aliachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni na Hakimu Mkuu wa Nakuru, Bi Elizabeth Usui, kwa makosa mawili yaliyohusiana na matamshi ya chuki.

Alishtakiwa kutumia lugha ya matusi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta.Jana, mbunge wa kapseret, Oscar Sudi alijisalimisha polisi kutokana na madai sawa na hayo.

You can share this post!

Huyu Mutua ni twiga, amejitokeza ChapChap!

Lazima niwanie urais 2022 – Kalonzo