• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:25 PM
Kesi ya Sonko yasikizwa faraghani

Kesi ya Sonko yasikizwa faraghani

Na RICHARD MUNGUTI

KESI ya ufisadi wa Sh10 milioni dhidi ya Gavana Mike Sonko na washtakiwa wengine wawili Antoy Ombok Otieno na kampuni ya ROG Securities Jumatatu ilianza kusikizwa faraghani baada ya mahakama kukataa ombi la kuisitisha kusubiri uamuzi wa mahakama kuu.

Bw Otieno aliwasilisha Ijumaa ombi katika Mahakama kuu akiomba hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Douglas Ogoti aagizwe asiendelee na kesi hiyo ya tatu dhidi ya Gavana Sonko, Otieno na ROG.

Watatu hao walikanusha mashtaka 13 baada ya korti kukataa kusitisha kesi hiyo kusubiri uamuzi wa Jaji Mumbi Ngugi aliyeratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura.

Ombi la kusitishwa kwa kesi hiyo liliwasilishwa na wakili Danstan Omari aliyeomba hakimu aahirishe kesi hiyo hadi Mahakama kuu itoe uamuzi ikiwa watatu hao walishtakiwa kwa njia inayofaa.

Viongozi wa mashtaka James Kihara na Irungu Gitonga walipinga ombi hilo wakisema “Jaji Ngugi alikataa kuisitisha kesi hiyo.

Wakili Cecil Miller akimtetea Gavana Sonko. PICHA/ RICHARD MUNGUTI

Bw Ogoti aliwaagiza viongozi wa mashtaka Mabw James Kihara na Irungu Gitonga wawasilishe ushahidi katika kesi hiyo Bw Sonko, Bw Ombok baada ya kusomewa mashtaka 13.

Bw Ogoti alitupilia mbali ombi la Bw Otieno na ROG la kusitisha kesi dhidi yao pamoja na Bw Sonko akisema “mahakama kuu haijatoa maagizo kuisimamisha.”

Hakimu alisema iwapo mahakama kuu itatoa maagizo ya kusimamishwa kusikizwa kwa kesi hiyo bila shaka itakoma kuendelea na kesi hiyo.

Akiwasilisha ombi hilo la Bw Otieno na ROG,Bw Omari alisema wawili hao hawakuelezwa awali kabla ya kufunguliwa kwa shtaka.

“Naomba hii mahakama itilie maanani Kifungu nambari 89 (5) cha sheria za uhalifu na kufikia uamuzi kuwa mashtaka dhidi ya washtakiwa hayana mashiko kisheria,” alisema Bw Omari.

Bw Omari alisema kesi hiyo iliratibishwa kuwa ya dharura na Jaji Ngugi na kuamuru isikizwe Jumatatu.

Hakimu mkuu Douglas Ogoti (kulia ameketi), washtakiwa Otieno Ombok na Gavana Mike Sonko. Picha/RICHARD MUNGUTI

Mahakama ilielezwa kuwa cheti cha mashtaka hakina mashiko kisheria kwa vile washtakiwa hawakuelezwa mashtaka yanayowakabili kabla ya kushtakiwa.

Bw Omari alisema wakenya zaidi ya 45milioni wanataka kujua hatma ya Sonko.

Wakili Cecil Miller aliongeza kumweleza hakimu kuwa afisi ya DPP ilikaidi agizo washtakiwa wapewe nakala za ushahidi katika muda wa masaa 36.

Akitoa uamuzi ,Bw Ogoti alikataa kusitisha kesi hiyo na kuamuru mashahidi watatu ambao majina ya yamefichwa waanze kutoa ushahidi kulingana na agizo la Mahakama kuu la Janauri 19,2020.

Mahakama kuu iliamuru mashahidi waliowekwa chini ya ulinzi watoe ushahidi faraghani.

You can share this post!

Jeraha lakomesha marejeo ya Arjen Robben

Obure na Ouko kujua hatima yao Jumatatu ijayo