• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 6:55 AM
BBI: Karua agonga Uhuru na Raila

BBI: Karua agonga Uhuru na Raila

Na RIPOTA WA TAIFA LEO

KIONGOZI wa Narc-Kenya, Martha Karua ametaja Mpango wa Maridhiano (BBI) kama njama kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga kutimiza maslahi yao ya kibinafsi ya kugawana madaraka.

Kwenye mahojiano na kituo cha habari cha Elephant, Bi Karua alisema wawili hao wameonyesha unafiki mkubwa huku nia yao kuu ikiwa ni kutafuta mbinu za mkato kugawana mamlaka.

“Rais na Raila hawajitokezi wazi kuhusu BBI. Wanawaeleza Wakenya machache kuhusu mpango huo tu badala ya kuweka wazi ripoti kamili,” akasema Bi Karua.

Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakisema kuwa BBI ni njia waliyokubaliana kutumia walipoingia handisheki kwa ajili ya kuunganisha Wakenya na kumaliza mizozo wakati wa uchaguzi.

Mwaka jana kamati hiyo ilitoa ripoti ya mapema iliyopendekeza kuongezwa kwa nyadhifa kuu za uongozi wa nchi zikiwemo waziri mkuu na manaibu wake.

Kulingana na Rais Kenyatta na Bw Odinga, ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa nchini kila wakati wa uchaguzi zinatokana na hali ambapo wanaoshinda wanachukua madaraka yote na kuwafungia nje wanaoshindwa.

Lakini Bi Karua alipuuzilia mbali kauli hiyo akisema BBI itasababisha migawanyiko zaidi baina ya Wakenya kwani inalenga kunufaisha wachache walio madarakani.

“Huu ni mpango wa kuvunja wala sio kuunganisha. Tayari BBI imegawanya wananchi. Inaongozwa na maslahi ya kibinafsi,” akasema.

Alieleza kuwa Wakenya hawajasema kuwa wanataka mabadiliko ya Katiba mbali ni Rais Kenyatta na Bw Odinga ambao wanaopendekeza marekebisho hayo.

“BBI haina chochote kuwahusu Wakenya. Huu ni mpango baina ya watu wawili ambao wanaendesha nchi hii. Watu hao ni Rais na Raila. Wakenya hawajasema wanataka Katiba irekebishwe.

“Katiba ya 2010 ilikuwa ya wananchi na matatizo yanayokumba Kenya hayatokani na udhaifu wake,” akasema Bi Karua.

Alimlaumu Rais Kenyatta akisema ndiye wa kulaumiwa kuhusu matatizo yaliyopo nchini kwa kukosa kutekeleza Katiba kikamilifu na kutozingatia utawala wa kisheria.

“Katiba ya 2010 haijazuia ustawi na maendeleo ya Kenya. Tatizo ni Serikali kupuuza Katiba hiyo kwa kukosa kuweka mbele maslahi ya wananchi,” akasema.

Bi Karua aliwahimiza Wakenya kukataa marekebisho yoyote ambayo lengo lake ni kunufaisha viongozi wakuu pekee.

“Wakenya wanapasa kusimama imara kupinga mchakato wowote ambao utavuruga Katiba,” akaeleza.

Pia alilaumu chama cha ODM akisema kimewasaliti Wakenya kwa kuingia kwenye ushirikiano na Serikali badala ya kutekeleza wajibu wake wa kukosoa serikali.

“Kwa kuingia kwenye serikali, ODM imefanya serikali kukosa kuwajibika. Wabunge wake wanapasa kuondoka kwenye vyeo vya kamati za kutathmini utendakazi wa serikali na kuacha wabunge wa vyama ambavyo havimo serikalini kuvikalia,” akaeleza.

Kuhusu ufisadi, Bi Karua alieleza kuwa inasikitisha kuwa walio madarakani na washirika wao wanaendelea kupora mali ya umma huku wananchi wakiendelea kuteseka kutokana na umaskini, magonjwa na ukosefu wa kazi.

“Ni jambo la kusikitisha sana kuwa watu hata wanaiba pesa za kukabiliana na corona na kuweka maisha ya wengi katika hatari,” akasema.

You can share this post!

Liverpool kutwaa huduma za Thiago kipindi cha lala salama

Wazee wa Kaya watisha kumlaani Jumwa kwa kumtetea Sudi