• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Watu 8 wauawa katika mapigano ya Legio Maria

Watu 8 wauawa katika mapigano ya Legio Maria

NA IAN BYRON

IDADI ya waliokufa kwenye fujo kati ya makundi mawili ya waumini wa dhehebu la Legio Maria katika Kaunti ya Migori imefika wanane.

Wanane hao walikufa kufuatia makabiliano makali katika madhabahu ya Got Kwer.

Papa Lawrence Kalul, ambaye anaongoza kundi lenye makao makuu katika Got Kwer, alisema watoto wawili pia hawajulikani waliko kufuatia ghasia hizo za Jumatatu.

Kufikia Jumatatu jioni watu watano walithibitishwa kuuawa kutokana na majereha ya risasi baada ya polisi kuingilia kati kuzima fujo kati ya waumini.

Watu wengine kadhaa walijeruhiwa akiwemo afisa wa polisi.

Hapo jana, waumini ambao walikesha katika madhabahu hayo walianza kuondoka wakihofia mashambulizi zaidi.

Kamanda wa polisi Kaunti ya Migori, Manaseh Musyoka, alisema waliouawa Jumatatu walipigwa risasi walipovamia polisi waliokuwa wametumwa kuzima fujo hizo.

Ghasia hizo zilizuka baada ya kundi linaloongozwa na Papa Raphael Adika kuingia katika madhababu hayo, ambamo tayari kundi la Papa Kalul lilikuwa likiendelea na ibada.

Papa Adika akiwa ameandamana na wafuasi wake chini ya ulinzi wa polisi walipofika walipata kundi la Papa Kalul likiwa tayari kwa silaha.

Ghasia zilizuka na na kulazimu polisi kufyatua hewa ya kutoa machozi na risasi kutuliza hali,

Kadinali Chamalengo Ong’aw alidai kuwa Papa Adika na kundi lake walikuwa wakitaka kufukua na kubeba mwili wa mwanzilishi wa dhehebu hilo, Melkio Ondetto, ambao umezikwa Got Kwer.

Kwa upande wake, Papa Adika alilaumu kundi pinzani akisema alikuwa akiwaongoza waumini wanaomuunga mkono kufanya maombi.

“Nilikuwa nimeenda kwa ajili ya maombi pamoja na waumini wenzangu lakini tukakaribishwa kwa fujo,” akasema.

Mzozo wa uongozi katika dhehebu hilo maarufu maeneo ya Nyanza ulianza 1992 kufuatia kifo cha Ondetto.

Mwezi uliopita, Papa Adika alienda kortini kupinga Kalul kutawazwa Papa.

You can share this post!

Mahabusu zaidi wahepa seli za polisi katika hali ya...

SAFARI RALLY: Barabara za Kenya zahitaji ujasiri, wasema...