Habari Mseto

Mgomo wasukuma wagonjwa kufurika hospitali ya misheni Baringo

September 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na Florah Koech

MAMIA ya wagonjwa katika Kaunti ya Baringo wamemiminika katika hospitali ya kimisheni eneo la Eldama Ravine, baada ya kukosa huduma katika vituo vya afya vya umma kwa sababu ya mgomo wa wauguzi.

Kulingana na Mercy Koech, msimamizi wa hiyo kwa jina Mercy Mission Hospital, tangu mgomo uanze, wamekuwa wakipokea wagonjwa, wengi wao wakiwa wagonjwa wanaotaka huduma za dharura.

“Tunapata zaidi ya idadi inayotarajiwa ya wateja hasa idara ya uzazi. Chumba cha kina-mama kujifungua kimejaa kwa sababu idadi ya wanawake wanaotafuta huduma imeongezeka mara tatu na hii imezidi uwezo wetu wa vitanda. Wagonjwa wanaomiminika katika kituo hiki ni wengi sana ikilinganishwa na idadi ya madaktari kiasi cha wengi kukosa wakati wa kupumzika,” akasema Bi Koech.

Idadi ya waliolazwa imepanda kutoka wagonjwa watatu kwa siku hadi zaidi ya 15 na wengi wao wanatoka Tiaty, Kabartonjo, Kabarnet, Kamara, Marigat na Londiani.

“Wauguzi wetu na madaktari hapa wamelazimika kufanya kazi kwa muda wa ziada na tumewaita wale walio likizo,” akasema.

Mgonjwa katika chumba cha wajawazito, Bi Monica Barkoton, alieleza alivyosafiri kutoka Bonde la Kerio baada ya kushindwa kukusanya zaidi ya Sh30,000 za kufanyiwa upasuaji katika kituo cha kibinafsi mjini Nakuru.

“Nilikuwa na maumivu ya uzazi lakini nilipopelekwa katika hospitali ya Kabarnet, haikuwa na mtu yeyote wa kunihudumia. Nikapelekwa kituo cha kibinafsi cha Nakuru lakini siku za pesa walizohitaji. Ndipo nilipoletwa haapa,” akasema.

Hildah Todoreng, mama wa watoto wawili, kutoka Barpello huko Tiaty aliletwa katika kituo hicho na kasisi mkatoliki baada ya kushindwa kupata msaada katika zaidi ya vituo vitatu vya umma kaunti hiyo.

“Nilikwenda kwa zahanati ya Barpello kujifungua lakini nikapelekwa kituo cha Afya Chemolingot ambacho kiko zaidi ya kilomita 70. Hakukuwa na dawa huko Chemolingot na niliamriwa kutoa Sh6, 000 kwa gari la wagonjwa ili nipelekwe hospitali ya Mercy. Sikuwa na yeyote na kasisi alinisaidia,” akasema Bi Todoreng ambaye ni mama wa watoto wanne.