• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Korane gavana wa sita kusimamishwa na korti kwenda ofisini

Korane gavana wa sita kusimamishwa na korti kwenda ofisini

Na RICHARD MUNGUTO

GAVANA Ali Korane ndiye kinara wa sita wa serikali za kaunti kupigwa marufuku kurudi afisini baada ya kushtakiwa kwa ubadhirifu wa zaidi ya Sh233milioni zilizotolewa na Benki ya Dunia kufadhili miradi ya maendeleo katika kaunti hiyo.

Bw Korane amejiunga na Magavana Moses Lenolkulal (Samburu), Mike Sonko (Nairobi), Okoth Obado (Migori) na Muthomi Njuki (Tharaka-Nithi) na aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu Baba Yao waliokatazwa kuingia tena afisini hadi kesi za ufisadi zinazowakabili sizikizwe na kuamuliwa.

Bw Korane alizuiliwa kurejea afisini na hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bwe Douglas Ogoti aliposhtakiwa katika kesi ya ufisadi.

Mbali na Gavana huyo maafisa wengine wanne wanaohudumu katika idara ya fedha pia walipigwa marufuku kurudi afisini hadi kesi inayowakabili isikizwe na kuamuliwa.

Watano hao ni Bw Korane, maafisa wakuu wa idara ya fedha Mabw Ibrahim Malow Nur almaarufu Ibrahim Malow Nur Shurie, Mohamed Ahmed Abdullah, Abdi Shalle Bure na Ahmed Abdallah Aden.

Wote walikanusha mashtaka ya kula njama za kufuja pesa za umma, kutozingatia sheria za uwekezaji na matumizi mabaya ya pesa.

Kulingana na mashtaka yaliyowasilishwa kortini na naibu wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma (ADPP) Alexander Muteti watano hao walifuja pesa hizo zilizonuiwa kufadhili ustawishaji wa kaunti ya Garissa.

Kupitia kwa mawakili Ahmednassir Abdullahi na Paul Nyamondi washtakiwa hao waliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana baada ya kukesha katika kituo cha polisi kilichoko afisi za tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC).

Mahakama ilifahamishwa washtakiwa walitekeleza makosa hayo kati ya Feburuari 25 na Septemba 30 2019.

Bw Korane aliachiliwa kwa dhamana ya Sh3,250,000 na wenzake wakapewa dhamana ya Sh1.2milioni. Dhamana zote ni pesa tasilimu.

Hakimu mkuu Douglas Ogoti (kulia). Picha/RICHARD MUNGUTI.

Shtaka dhidi watano hao lilisema walikula njama za kutumia vibaya pesa zilizokuwa zimetengewa ustawishaji wa jiji la Garissa katika utengenezaji mitaro na barabara (KUSP)

Mahakama ilielezwa na Bw Muteti kuwa Bw Korane alikaidi sheria za kusimamia barabara pesa hizo.

Ibrahim na Mohamed walishtakiwa pamoja kuidhinisha kuondolewa kwazaidi ya Sh205milioni kutoka akaunti ya Benki kuu ya Kenya (CBK) hadi benki ya Equity (EBL).

Pesa hizo ziliwekwa katika akaunti ya Garissa Urban Institutional Grant katika benki ya EBL.

Bule na Ibrahim walishtakiwa kupeleka Sh21,663,000 idara ya Afya.

Aden na Bule walishtakiwa kuhamisha Sh2milioni hadi akaunti ya Afya inayofadhiliwa na mashirika ya ufadhili miradi ya maendeleo.

Pia wawili hao walishtakiwa kwa kuhamishwa Sh30milioni kutoka KUSP hadi idara ya ustawishaji maji.

Shtaka lingine dhidi ya Ibrahim, Bure na Aden lilisema walihamishwa Sh30m kutoka akaunti ya KUSP hadi akaunti ya ustawishaji mitaro ya uondoaji maji taka.

Akiwasilisha ombi la kuachiliwa kwa dhamana, Bw Abdullahi alisema hakuna pesa zilizopotea mbali zingali katika kaunti hiyo.

Bw Abdullahi alisema washtakiwa hawakufanya makosa kwa vile hakuna ushahidi wowote uliotolewa kuthibitisha pesa hizo ziliibwa ama kutoweka katika akaunti za kaunti hiyo.

“Pesa hizi zingali katika akaunti ya Garissa,” alisema Bw Abdullahi akiongeza, “ hakuna pesa zilizowafaidi washtakiwa hawa.”

Akitoa uamuzi Bw Ogoti alisema hakuna ushahidi Gavana huyo alijinufaisha na pesa hizo zilizotolewa na WB kufadhili miradi ya ustawishaji kaunti hiyo.

You can share this post!

Meneja wa zamani apatwa na hatia ya kutafuna Sh62.7 milioni

Aubameyang kusaidia Arsenal kufuma mabao hadi 2023