• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wanaonyemelea vipande vya ardhi ya umma waonywa Kwale

Wanaonyemelea vipande vya ardhi ya umma waonywa Kwale

Na MISHI GONGO

GAVANA wa Kaunti ya Kwale Salim Mvurya amewaonya wanaovamia misitu ya kaya na ardhi za umma katika kaunti hiyo, akisema kuwa kufanya hivyo kunalemaza juhudi za kutunza mazingira na tamaduni.

Bw Mvurya alisema kaya zinaumuhimu kubwa kwa jamii ya wamijikenda na ilistahili kutunzwa.

“Sehemu hizi zina umuhimu mkubwa kwa jamii za watu wa Pwani. Ni sehemu zilizo na kumbukumbu ya maisha ya watu wa hapa na zinastahili kuhifadhiwa. Ni hatia kwa mtu kunyakuwa,” akasema.

Mwezi Julai wazee wa kaya Tiwi waliiomba serikali kuingilia kati kusimamisha ujenzi wa ukuta katika kaya hiyo uliokuwa unafanywa na mtu binafsi.

Walisema licha ya mahakama kutoa agizo la kusimamisha ujenzi wa aina yoyote kwa ardhi hiyo, muekezaji mmoja wa kibinafsi aliendeleza ujenzi wa ukuta.

Kaya Tiwi na Kaya Kinondo ziko karibu na fuo ya bahari katika eneo la Diani hivyo kuzifanya kuwa katika tishio la kunyakuliwa na matajiri.

Alisema Kaya hizo mbili zimesajiliwa kuwa miongoni mwa makavazi ya kitaifa.

Gavana huyo alisema waekezaji wa kibinafsi wameanza kunyemelea misitu ya kaya hizo.

“Katika uongozi wangu nataka kuwahakikishia misitu ya kaya itasalia kuwa mali ya serikali na kuwa hakuna mtu atainyakua,” akasema.

Aliongezea kusema kuwa atarudisha vipande vyote vya ardhi vilivyonyakuliwa katika kaunti hiyo kwa mikono ya serikali.

“Kuna baadhi ya wawekezaji ambao wameanza kunyemelea ardhi za umma wakidhani kuwa hawatatambulika; nataka kuwaambia kuwa chuma chao kimotoni. Wenyeji na wawekezaji wote wanapaswa kufuata sharia za nchi,”akasema.

You can share this post!

Je, una maoni gani kuhusu chupi?

Mamlaka ya KNQA yakagua MKU