Gor Mahia yamkweza Oluoch kuwa kocha wa makipa
Na CHRIS ADUNGO
NAHODHA wa zamani wa Gor Mahia, Jeremy Onyango, amekwezwa ngazi kuwa kocha wa makipa wa kikosi cha kwanza cha mabingwa hao mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL).
Hadi kuteuliwa kwake, Onyango alikuwa mkufunzi wa makipa chipukizi wa Gor Mahia. Mlinda-lango huyo wa kimataifa aliingia katika sajili rasmi ya Gor Mahia mnamo 2008 na akawachezea hadi 2017 alipostaafu soka.
Japo alitamani kujitosa katika ulingo wa siasa, Onyango alipokezwa ukocha wa makipa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 17 kambini mwa Harambee Stars. Sasa anajaza pengo la Willis Ochieng aliyejiunga na Gor Mahia mnamo 2017 baada ya kutokea Zoo FC kuwa kizibo cha aliyekuwa kipa matata wa kimataifa, Matthews Ottamax.
“Usimamizi wa Gor Mahia umeamua kumkweza Onyango kutokana na matokeo bora ambayo amekuwa akisajili kambini mwa kikosi chipukizi. Amefanya kazi nzuri na ameridhisha pia katika timu ya taifa ya U-17,” akasema mwekahazina wa Gor Mahia, Dolfina Odhiambo.
“Tulifungwa idadi kubwa ya mabao katika kipindi cha misimu miwili iliyopita. Hii ndiyo sababu iliyochochea uteuzi wa Onyango ambaye tunaamini atarejesha uthabiti katika idara hiyo. Tunamtakia Ochieng kila la heri katika mustakabali wake kitaaluma na tunamshukuru kwa mchango wake akiwa nasi,” akaongeza kinara huyo.
Wakati uo huo, Posta Rangers wako pua na mdomo na kumsajili fowadi Dennis Oalo kutoka kambini mwa Gor Mahia.
Kocha Sammy ‘Pamzo’ Omollo wa Rangers amesema kwamba kikosi chake kimekuwa kikimvizia Oalo kwa kipindi kirefu na dalili zote zinaashiria kwamba atakuwa mchezaji wao msimu ujao wa 2020-21.
Oalo alijiunga na Gor Mahia mnamo Julai 2019 baada ya kuagana na kikosi cha Nairobi Stima katika Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL). Ingawa hivyo, alisalia kusugua benchi katika mechi nyingi za msimu uliopita baada ya kushindwa kumudu ushindani mkali kutoka kwa washambuliaji Nicholas Kipkirui, Juma Balinya na Gislein Yikpe.
“Mazungumzo kati ya Rangers na Oalo yako katika hatua muhimu na tunatarajia kwamba sogora huyo atatia saini mkataba atakapokezwa na klabu wiki hii. Ujio wa Oalo utaleta nguvu mpya katika safu ya mbele na kuinua viwango vya ushindani,” akasema Pamzo.
Rangers wamefichua pia azma ya kusajili wanasoka wawili zaidi muhula huu ili kupiga jeki safu yao ya kati. Hadi kufikia sasa, kikosi hicho tayari kimesajili wanasoka Tom Onyango na Salim Hamisi kutoka Chemelil Sugar na Western Stima mtawalia.
“Hatutajishughulisha sana sokoni muhula huu kwa sababu tumefaulu kudumisha kambini idadi kubwa ya wanasoka tuliowategemea katika msimu uliopita. Tunapania kujaza mapengo ya wanasoka watano pekee walioagana nasi mwishoni mwa msimu wa 2019-20,” akasema Pamzo ambaye ni mchezaji wa zamani wa Harambee Stars.
Pamzo ambaye pia amewahi kuwa kocha wa Tusker FC, amefichua kwamba waajiri wao wameazimia kulipa malimbikizi yote ya mishahara ya tangu Machi 2020 kufikia mwisho wa wiki ijayo.