• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Kaunti zote zitapokea fedha Jumatatu – Serikali

Kaunti zote zitapokea fedha Jumatatu – Serikali

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Fedha Ukur Yatani Ijumaa alisema kuwa serikali 47 za kaunti zitasambaziwa Sh60 bilioni kuanzia Jumatatu, Septemba 21, 2020.

Hii ni baada ya maseneta kukubaliana Alhamisi jioni kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha baina ya kaunti, baada ya wao kuvutano kuhusu suala hilo kwa miezi mitatu.

Kwenye taarifa, Bw Yatani alisema pesa hizo ni sehemu ya Sh316.5 bilioni ambazo serikali za kaunti zilitengewa katika bajeti ya mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021.

‘Ningetaka kuwahakikishia Wakenya kwamba tutawasambaza pesa hizo kuanzia Jumatatu. Tumekamilisha mipango yote ndani ya Hazina Kitaifa. Fedha ziko tayari,” akasema.

Kulingana na sheria, Hazina ya Kitaifa haiweze kutoa fedha kutoka Hazina ya Pamoja (Consolidated Fund) bila idhini ya bunge la kitaifa.

Kwa hivyo, mfumo mpya wa ugavi wa fedha baina ya kaunti ambao ulipitishwa na maseneta Alhamisi unafaa kuidhinishwa kwanza katika Bunge la Kitaifa sawa na Mswada kuhusu Ugavi wa Fedha baina ya Kaunti (CARA).

Ni baada ya mswada huo kutiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta ambapo Hazina ya Kitaifa itakuwa huru kusambaza fedha kwa kaunti.

Ikizingatiwa kuwa Bunge la Kitaifa huwa hakifanyi vikao mnamo Jumatatu, hii ina maana kuwa shughuli hiyo itakamilishwa mnamo Jumanne, alasiri.

Kwa hivyo, sheria hiyo itawasilishwa kwa Msimamizi wa Bajeti (CoB) ambaye ndiye atatoa idhini kwa Hazina ya Kitaifa isambaze fedha kwa kaunti.

You can share this post!

Maseneta wamlaumu Gavana Wambora kuhusu usimamizi wa fedha...

Kisumu All Stars kutaja benchi mpya ya kiufundi