• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 6:55 AM
Raila aonya BBI ikipuuzwa umaskini utaongezeka Kenya

Raila aonya BBI ikipuuzwa umaskini utaongezeka Kenya

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, ameonya kuwa mizozo iliyoshuhudiwa baina ya viongozi kuhusu ugavi wa fedha kwa kaunti ni dalili ya vita siku za usoni ikiwa Mpango wa Maridhiano (BBI) utapuuzwa.

Bw Odinga alidai kuwa, nchi ya Kenya imo hatarini kujipata vitani kwa sababu ya umaskini unaozidi kuongezeka katika jamii.

Kulingana naye, dawa ya kuepusha hali hii kutokea siku za usoni ni kupitisha mapendekezo yatakayotolewa kwenye ripoti inayosubiriwa ya BBI.

Ripoti hiyo inayotarajiwa, itahitaji wananchi kushiriki kura ya maamuzi kurekebisha katiba.Bw Odinga alisema mvutano ulioibuka kwa wiki kadha kuhusu ugavi wa rasilimali kwa serikali za kaunti ulidhihirisha kuna masuala mazito ambayo ni sharti taifa litatue kwa dharura.

Kulingana naye, ni wazi kuwa nchi imeshindwa kutumikia mahitaji ya wananchi ambao idadi yao inaongezeka kwa kasi kwa vile hakuna rasilimali za kutosha.

Watu wanalazimika kupigania rasilmali chache zinazopatikana, kwa mujibu wa Bw Odinga.

“Ni lazima nchi hii, kwa dharura, ianze kujadili jinsi itakavyotoa nafasi sawa kwa kila Mkenya kushiriki kikamilifu katika ustawishaji wa nchi ili kwa pamoja tuzalishe kiwango cha utajiri kitakachotosheleza mahitaji yetu yote,’ akasema kwenye taarifa.

“Hili lisipofanywa, hasa kwa kuzingatia idadi inayoongezeka kwa kasi ya vijana walio na elimu, tutakuwa na vita vibaya zaidi katika siku zijazo tukitaka kugawa umaskini wetu badala ya utajiri,’ akaongeza.

Ripoti ya utafiti iliyotolewa majuzi na Idara ya Takwimu za Kitaifa (KNBS), ilionyesha kuna takriban Wakenya milioni 15.9 ambao ni maskini, kati ya jumla ya Wakenya milioni 44.2.

Katika takwimu hizo, mtu maskini alitajwa kama anayepokea chini ya Sh3,252 kila mwezi akiishi mashambani au Sh5,995 akiishi mjini.

Walio maskini pia walitajwa kama wanaokosa mahitaji muhimu ya kimaisha au huduma bora ikiwemo chakula, afya, elimu, habari, maji, usafi na makao.

Taarifa ya Bw Odinga ilitolewa siku moja baada ya maseneta kukubaliana kuhusu mfumo ambao utatumiwa kugawa fedha kwa kila kaunti katika kipindi cha fedha cha mwaka huu.

Maseneta walikuwa wametofautiana kwa vile mfumo uliopendekezwa awali ungesababisha baadhi ya kaunti maskini kupunguziwa fedha.

Iliamuliwa hakuna kaunti itakayopokea kiwango kidogo cha fedha kuliko ilivyopokea mwaka uliopita.Balozi huyo wa masuala ya miundomsingi katika Muungano wa Afrika (AU) alieleza kuwa, BBI itatoa nafasi mwafaka kwa taifa kuongeza uzalishaji wa rasilimali na ugavi sawa kwa kila eneo na kupiga vita ufisadi.

“Ni matarajio yangu kuwa sasa nchi inaweza kuelekeza mawazo yake katika mapendekezo ya mageuzi ambayo yanalenga kuzidisha ustawishaji,” akasema.

Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga husisitiza katiba inafaa kurekebishwa ili kutatua changamoto zinazokumba nchi kama vile ukabila na umaskini.

Kwa upande mwingine, wanaopinga kura ya maamuzi akiwemo Naibu Rais William Ruto hudai ni njama ya kunufaisha watu wachache kisiasa.

You can share this post!

Wataalamu washutumu vyuo vikuu kwa kutoa mafunzo duni

Corona: Watu 40 kushiriki majaribio ya chanjo Kenya