• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
Kizungumkuti cha Mukhisa Kituyi katika uchaguzi wa 2022

Kizungumkuti cha Mukhisa Kituyi katika uchaguzi wa 2022

Na CHARLES WASONGA

UJIO wa Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD), Dkt Mukhisa Kituyi katika kinyang’anyiro cha urais cha mwaka 2022 unatarajiwa kuvuruga hesabu za vigogo ambao wametanga azma ya kuwania wadhifa huo.

Wao ni Naibu Rais William Ruto, Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Alfred Mutua (Maendeleo Chap Chap) miongoni mwa wengine.

Hii ni kutokana na sababu kwamba Dkt Kituyi si mgeni katika ulingo wa siasa na serikali kwani amewahi kuhudumu kama mbunge na waziri katika enzi ya tawala za marais wa zamani marehemu Daniel Moi na Mwai Kibaki.

Alichaguliwa kama Mbunge wa Kimilili katika uchaguzi wa kwanza baada ya kurejelewa mfumo wa vyama vingi nchini, 1992 kwa tiketi ya Ford Kenya.

Alikuwa miongoni mwa kundi la wanasiasa vijana, nyakati hizo, almaarufu Young Turks waliopigania mageuzi ya Katiba hasa kuondolewa kwa mfumo wa utawala wa chama kimoja.

Vilevile, Dkt Kituyi alihudumu kama Waziri wa Biashara na Viwanda kati ya miaka ya 2002 na 2007 kabla ya kuteuliwa kuwa mshauri wa masuala ya utawala na biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Afrika.

Aliteuliwa katika kuwa Katibu Mkuu wa saba wa UNCTAD mnamo Septemba 1, 2013 na na mnamo Julai 2017 aliongezewa kipindi kingine cha miaka mitano ambacho kinamalizika mnamo Julai 30, 2021.

Mbali na tajriba hii katika ulingo za siasa na utawala, humu nchini na katika ngazi za kimataifa, hali ambayo imefanya nyota yake kung’aa zaidi, ni minong’no kwamba huenda Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga wakakubaliana kumuunga mkono Dkt Kituyi kama “mgombeaji wa handisheki”.

Hii ni kwa sababu mwanadiplomasia huyu ni “safi” na hajazingirwa na wanasiasa fisadi sawa na wagombeaji wengine.Itakumbukwa kuwa akiwa bungeni na serikalini, Dkt Kituyi alikuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanamsawiri kama mtu ambaye hawezi kuchochea joto la kisiasa nchini kuelekea uchaguzi mkuu ujao na hivyo kutikisa uthabiti wa nchi.

“Nadhani Dkt Kituyi ndiye mgombeaji Rais Uhuru Kenyatta alikuwa akirejelea mnamo Novemba 1, 2018 akiwa Nyeri aliposema kuwa chaguo lake litawashangaza wengi. Hana doa la ufisadi kama wagombeaji wengine ambao wanaonekana kuwa na ufuasi mkubwa; na Rais Kenyatta atakuwa amelitendea taifa hili hisani kubwa ikiwa atampendekeza Kituyi kama mrithi wake,” anasema Martin Andati.

“Nafahamu kwamba mazungumzo yamekuwa yakiendelea katika majukwaa mbalimbali, hata miongoni mwa washirika wa karibu wa rais kuhusu haja ya kuwepo kwa mgombeaji mbadala. Nadhani jina la Dkt Kituyi ni miongoni mwa yale ambayo yamekuwa yakitajwa,” anaongeza mchanganuzi huyo.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Bw James Mwamu ambaye anaongeza kuwa Dkt Ruto na Bw Odinga ambao ndio sasa wanaonekana kifuwa mbele katika kinyang’anyiro cha urais 2022 wanaweza kuchochea uhasama mkubwa nchini.

“Taifa hili linahitaji mgombeaji urais asiyeweza kuchochea msisimko mkali kama ambavyo tumeshuhudia kwa Naibu Rais na Bw Odinga. Linahitaji mgombeaji asiweza kuchochea hisia potovu za kikabila na bila shaka asiyejinasibisha na wanasiasa wafisadi,” anasema mdadisi huyu ambaye pia ni wakili.

Kwenye mahojiano katika kituo kimoja cha redio nchini (Redio Jambo) hivi majuzi Dkt Kituyi aliungama kuwa anajitosa katika kinyang’anyiro cha urais 2022 na kwamba tayari amebuni sekritaria ya kushirikisha kampeni zake. Hata hivyo, hakukana wala kukubali kuwa “mradi” wa Rais Kenya na Bw Odinga.

“Baada ya kukamilisha muhula wangu wa pili na wa mwisho katika UNCTAD, nataka kusaka nafasi ya kuwa katika nafasi kutatua changamoto za nchi hii katika ngazi ya kitaifa. Nataka kuleta mwamko mpya katika uongozi nchini bila kuvuga ufanisi ambao umefikiwa na serikali ya sasa,” akasema.

Dkt Kituyi akaongeza: “Nina tajriba kubwa katika ulingo wa uongozi kimataifa. Nimejenga mahusiano katika zaidi ya mataifa 119 kote ulimwenguni nikitekeleza wajibu wangu katika shirika hilo la Umoja wa Mataifa (UN). Nadhani tajriba hii inaweza kufaidi taifa langu ambako nimehudumu kama mbunge kwa miaka 15 na waziri kwa miaka mitano.”

Japo aliungama kuwa na “uhusiano mzuri” na Rais Kenyatta na Bw Odinga, Dkt Kituyi alisema anawania urais kwa misingi ya maono na sera wala “sio kwa sababu ya kusukumwa na mtu fulani.

“Nikigombea wadhifa huo, sidhani kama ninafanya hivyo kwa sababu mimi ni silaha au mradi wa mtu fulani. Kwangu sitegemei kuwa kusukumwa na mtu. Isitoshe, nitawania kwa chama tofauti kabisa kisichokuwa na uhusiano na Jubilee wala Nasa,” akasema.

Dkt Kituyi alisema kuwa huwa anashauriana kwa kina na Rais Kenyatta na Bw Odinga, anavyofanya na wagombeaji wengine kama vile Mbw Mudavadi na Musyoka.

“Nina uhusiano mzuri zaidi na Rais Kenyatta. Na hushauriana naye kuhusu jinsi UN inavyoweza kufaidi Kenya. Naye Raila amekuwa rafiki yangu kwa miaka mingi tangu miaka ya 1990s tulipokuwa tukipigania ukombozi wa pili nchini. Huwa tunajadili masuala mengi yanayolenga kuboresha taifa hili,” akaeleza.

Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe alisema kuwa japo amekuwa akimpigia debe Bw Odinga kama mgombeaji aliyehitimu kumrithi Rais Kenyatta, Dkt Kituyi “pia ni miongoni mwa wagombeaji bora”.

“Namfahamu zaidi Dkt Kituyi. Tulihudumu naye katika bunge la nane na ni kiongozi shupavu,” akasema.Ikiwa atagombea urais 2022, Dkt Kituyi anaungana na wengine ambao wametumia nyadhifa zao kama katika ngazi ya kimataifa na Afrika kama ngazi ya kuwawezesha kugombea urais katika mataifa yao.

Kwa mfano, aliyekuwa Rais wa Malawi Mbingu wa Mutharika alitumia cheo chake kama Katibu Mkuu wa soko la pamoja la Afrika Mashariki na Kusini (COMESA) kama kichochea cha kuwania urais na akashinda.

Naye aliyekuwa Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf alitumia nafasi yake kama naibu katibu mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Afrika (UNDP) kama msingi kuwania urais na akashinda. Je, Kituyi ataiga mfano wa wawili hawa?

You can share this post!

Rais anavyozua taharuki kuhusu hatima yake ya kisiasa

Tempes kijana anayeandaliwa kuwarithi Ole Ntimama na...