Siasa

Tempes kijana anayeandaliwa kuwarithi Ole Ntimama na Nkaisery Umaasaini

September 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na WANDERI KAMAU

JAMII ya Wamaasai imeanza harakati za kutafuta mrithi na msemaji wake kisiasa ielekeapo 2022, kwenye hatua inayolenga kuimarisha sauti na ushawishi wake kwenye siasa za kitaifa.

Jamii hiyo imekuwa kama “yatima” kisiasa tangu vifo vya viongozi wake, William Ole Ntimama mnamo Septemba 2016 na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Joseph Nkaissery mnamo Julai 2017.

Wawili hao ndio walikuwa wasemaji wakuu wa jamii hiyo kisiasa baada ya kifo cha aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof George Saitoti, kwenye ajali ya ndege katika msitu wa Ngong mnamo 2012.

Tangu kifo cha Bw Nkaissery, duru zinasema kuwa viongozi wa kidini na kitamaduni wamekuwa wakifanya vikao kutafuta kiongozi atakayeiunganisha jamii hiyo, ili kuondoa hali ya sasa ambapo inaonekana kuyumba kisiasa.

Ripoti zinaeleza kwamba baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakitajwa ni Gavana Joseph Ole Lenku (Kajiado) na Seneta Ledama Ole Kina (Narok).

Hata hivyo, upeo wa harakati hizo ulidhihirika Jumapili iliyopita, baada ya baadhi ya wazee na viongozi wa kidini kumtawaza Timothy Tempes, ambaye ni mwanawe Ntimama, kuwa msemaji maalum wa kisiasa wa jamii hiyo.

Mara tu baada ya kutawazwa, Tempes alisema kuwa yuko tayari kujaza nafasi iliyoachwa na babake, ili “kurejesha sauti ya Wamaasai kwenye maamuzi kuhusu uongozi nchini.”

“Nitafuata nyayo za babangu kuiunganisha familia yake na kutetea maslahi ya kaunti zote za jamii ya Wamaasai,” akasema Tempes, aliyeonekana kuzidiwa na hisia.Vile vile, alitangaza kuwania ubunge katika eneo la Narok Kaskazini “ili kumweka katika nafasi sawa kuendeleza utetezi wake.”

Kutokana na mwelekeo huo, wadadisi wa masuala ya sisasa wanasema kuwa ingawa huenda hilo likawa mwanzo mpya wa kisiasa kwa jamii ya Wamaasai, itakuwa vigumu kwa yeyote kurejesha ushawishi waliokuwa nao Ntimama na Nkaissery.

Hivyo, baadhi yao pia wanatilia shaka ikiwa viongozi wote walishirikishwa kwenye hafla, ikizingatiwa jamii hiyo hukita uongozi wake sana katika koo.

“Kwa muda mrefu, jamii ya Wamaasai imekuwa ikikita uongozi wake kwenye koo za Purko na Illmasai, kwani ndizo kubwa zaidi ikilinganishwa na zingine. Je, viongozi wake walishirikishwa kwenye maamuzi hayo? Hilo ndilo litakaloamua mwelekeo na hatima ya kutawazwa kwa mwanawe Ntimama,” asema Dkt Godfrey Sang’, ambaye ni mwanahistoria na mdadisi wa siasa.

Kwa mujibu wa wadadisi, mapokezi ya Tempes ndiyo yatakayoamua ikiwa “sauti ya Ntimama itarejea” hasa wakati ambapo viongozi kama Ole Kina wameibukia kuwa maarufu kutokana na misimamo yao kwenye masuala ya kitaifa na yale yanayohusu maslahi ya jamii hiyo.

Wadadisi wanasema kuwa mojawapo ya hali ambazo huenda zikaleta migongano ya kitamaduni kati ya Mabwana Kina na Tempes ni kuhusu koo wanakotoka.

Tempes anatoka katika ukoo wa Purko, ambao miongoni mwa koo kubwa na zenye ushawishi, huku Bw Kina akitoka katika ukoo wa Laigwanak, ambao ni miongoni mwa koo ndogo.

“Licha ya mikondo ya kimaisha na uongozi kubadilika pakubwa, jamii hii inazingatia sana masuala ya ukoo. Ukoo ndio msingi wake mkuu kimaisha. Ndio pia unaotoa mwelekeo kuhusu masuala mengine kama siasa na utamaduni,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa. Wadadisi pia wanataja mwelekeo wa siasa za 2022 kama utakaoathiri sana uongozi wake.

Hii ni ikizingatiwa kuwa baadhi ya viongozi wamegawanyika kati ya kambi inayomuunga mkono Naibu Rais William Ruto na nyingine inayoegemea upande wa handisheki, kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakimpigia debe Dkt Ruto katika eneo hilo ni Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Kajiado, Bi Mary Seneta.

Bi Seneta amekuwa akiongoza jumbe mbalimbali za jamii hiyo kukutana na Dkt Ruto katika makazi yake mtaani Karen, jijini Nairobi, ambako wamekuwa wakimhakikishia kumuunga mkono kuwania urais kwenye uchaguzi wa 2022.Viongozi wengine ambao wamehusishwa na kambi ya Dkt Ruto ni Gavana Samuel Tunai wa Narok.

Bw Odinga naye amekuwa akipokea jumbe kutoka eneo hilo zikiongozwa na Gavana Lenku kati ya viongozi wengine, ambapo kama Dkt Ruto, wamekuwa wakimhakikishia kumuunga mkono ikiwa atawania urais.

Kutokana na mielekeo hiyo, wadadisi wanasemaBw Tempes anakabiliwa na kibarua kizito kuiunganisha jamii hiyo kama walivyofanya watangulizi wake.Wanasema kuwa kinyume na sasa, ilikuwa rahisi kuiunganisha katika miaka ya themanini na tisini, kwani kwani Kanu ndicho kilikuwa chama pekee cha kisiasa.

“Kukiwa na mirengo shindani kisiasa kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga, hali ni tofauti sana na ilivyokuwa nyakati za viongozi kama Stanley Ole Tipis na Stanley Oloitiptip miaka ya themanini, kwani Kanu ndicho kilikuwa chama pekee cha siasa,” asema Bw Mutai.