Mbabazi akataa mahari kutoka kwa Ramaphosa
Kampala UGANDA
ALIYEKUWA waziri mkuu wa Uganda na mgombeaji wa urais Amama Mbabazi, amekataa mahari kutoka kwa familia ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ambaye mwanawe anataka kumuoa binamu wa mke wake.
Bw Mbabazi aliwaambia jamaa wa Rais Ramaphosa, ambao walikuwa wameandamana na Andile Ramaphosa kumposa Bridget Birungi Rwakairu, kwamba mazoea ya wazazi kubadilisha mahari na binti zao yanadunisha wanawake.
Bw Mbabazi alisema mali ambayo wazazi hutumia kuwalea watoto wao ni ya thamani kuu kiasi kwamba haiwezi kufananishwa na wanyama (mahari).
“Hatugawi binti yetu. Angali wetu, kwa hivyo kile ambacho mnatupa leo, tutaipa familia hii changa (wanaooana) ili iweze kuisaidia katika kujenga familia yake,” Bw Mbabazi ambaye alimlea Bi Rwakairu aliwaambia jamaa wa Rais Ramaphosa.
Ilikuwa imeripotiwa kwamba Bw Ramaphosa alitarajiwa kulipa ng’ombe 100 na zawadi nyingine katika sherehe ya mahari ya mwanawe Andile.
Bw Mbabazi alisema akiwa mmoja wa waandalizi wa katiba, walihakikisha kwamba wamekabili changamoto za ukosefu wa usawa wa jinsia ikiwemo ulipaji wa mahari.
Alisema ulipaji wa mahari umemkosesha mwanamke utu na kusababisha misukosuko katika familia kwa kufanya wanawake kuonekana kama mali ya wanaume.
“Hii ni aina ya dhuluma iliyokuwapo kabla ya historia kuanza kuandikwa na tunafaa kuimaliza. Tunafaa kuwa tukijenga uhusiano kati ya familia zote mbili na kukuza mizizi ya familia. Hatupeani binti yetu kwa sababu yeye angali mmoja wetu,” alisema.
Alisema hayo baada ya Bw Charles Mbire, aliyekuwa msemaji wa ujumbe wa familia ya Ramaphosa kusema kwamba walikuwa tayari kulipa mahari ili wapewe Bi Rwakairu.
Kauli ya Bw Mbabazi pia iliungwa na waziri mkuu wa sasa
Dkt Ruhakana Rugunda ambaye alikuwa upande wa Bi Rwakatiru. “Hatutaki kusikia neno mahari katika mkutano huu kwa sababu hatumuuzi binti yetu. Mnaweza kutumia neno nyingine.
Pengine mseme zawadi ya kuwashukuru sisi wazazi kwa kumzaa na kumlea binti yetu,” alisema Dkt Rugunda.
Familia ya Bw Mbabazi na ujumbe wa watu 12 kutoka Afrika Kusini ulioongozwa na Bi Hope Ramaphosa, mama ya bw harusi walikubaliana ngombe watano na mbuzi watano.
Ngombe hao walikabidhiwa Andile Ramaphosa na bibi yake mtarajiwa. Mbuzi hao walipatiwa shangazi na wajomba wa Rwakairu kama shukrani kwa kumlea.
Hata hivyo, jamaa za Rwakairu walimtoza Andile faini ya mbuzi mmoja kwa kuzaa mtoto na binti yao nje ya ndoa.
Andile na Rwakairu walikutana China wakiwa masomoni na wanatarajiwa kuoana rasmi mwishoni mwa mwaka huu.