Habari Mseto

Joho anyenyekea mbele ya madiwani

September 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

GAVANA Hassan Joho wa Mombasa ameanza mapatano na madiwani wa Mombasa baada ya malumbano yaliyoleta hisia kali katika bunge la kaunti.

Bw Joho pia alitangaza kuwa atawakaribisha madiwani hao kwenye mkutano wa kujadili masuala ya bunge hilo ili kumaliza mgogoro unaoendelea kutokota.

Hatua hiyo inajiri siku chache baada ya madiwani kutoa madai kuwa Bw Joho amekuwa akiingilia uongozi na maamuzi muhimu ya bunge la kaunti.

Baadhi yao walisema hawana uhuru wa kujadili hoja yoyote bila ya kibali cha Gavana Joho, jambo walilosema ni hujuma kwa uhuru wa bunge hilo.

Kwenye hotuba yake ya kwanza katika bunge la kaunti tangu mwaka 2019, Bw Joho aliwasihi madiwani wafanye kazi na serikali yake ili kuleta maendeleo kwa umma.

“Tusonge mbele kwa umoja na amani ili kuhakikisha miaka miwili iliyosalia tufanya mabadiliko na maendeleo kwa wakazi wa Mombasa, hususan kukabiliana na changamoto zinazokumba jiji letu,” Bw Joho alisema.

Pia aliwataka wawakilishi hao wapitishe miswada kadhaa ambayo serikali yake iliwasilisha bungeni.

“Tafadhalini nawarai mpitishe miswada hiyo na mingine ambayo tutawasilisha. Wakazi wanataka huduma na inatupasa tuwajibike. Dunia inafaa itambue uongozi wa Mombasa umekomaa kisiasa,” aliwabembeleza wawakilishi hao.

Haya yanajiri wiki moja baada ya wawakilishi hao kumlaumu kwa kuingilia maswala ya bunge.

Hata hivyo, mwakilishi wa wadi ya Freretown, Bw Charles Kitula alipuuzilia mbali hotuba ya Bw Joho ya kuleta mapatano akisema alikuwa akiwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

Bw Kitula alimtaka Bw Joho aeleze wakazi maendeleo aliyoyaleta katika uongozi wake tangu 2013 alipochaguliwa gavana wa kwanza wa Mombasa.

“Angetwambia maendeleo aliyoyafanya tangu achaguliwe kuwa gavana wala si masuala ya serikali kuu na urafiki wake na Rais Uhuru Kenyatta. Tunataka awajibike. Alikuja bungeni sababu ya joto la siasa,” akasisitiza Bw Kitula.