Habari Mseto

Pendekezo la Wandayi lazua mgawanyiko ODM

May 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RUSHDIE OUDIA

BAADHI ya viongozi wa ODM wamepinga pendekezo la Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi kwamba chama hicho kibadili sheria za uteuzi kwa kufutilia mbali kura za mchujo kwa wadhifa wa ugavana.

Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’ na Mbunge Mwakilishi wa kaunti hiyo Glady Wanga wanahisi kuwa hakuna haja kwa chama hicho kubadili sheria zake za uteuzi.

Badala yake wawili hao wanapendekeza kuwa shughuli hizo za kura za mchujo ziendeshwa kwa makini na uangalivu mkubwa ili kuondoa visa vya udanganyifu.

Wiki iliyopita Bw Wandayi alipendekeza kuwa ODM inapaswa kubuni jopo la kuwachunguza wanaotaka kuwania ugavana ambapo mmoja kati yao atateuliwa kushindana na wagombeaji kutoka vyama vingine katika katika uchaguzi mkuu ujao na chaguzi zingine zitakazotokea.

Mbunge huyo, ambaye pia ndiye Mkurugenzi wa Masuala ya Kisiasa katika chama hicho, anasema kufutiliwa mbali kwa mchujo wa ugavana kutaokoa rasilimali za ODM na kuondoa joto la kisiasa ambalo husababishwa na ushindani mkali wa tiketi ya wadhifa huo.

Bw Wandayi alisema atawasilisha pendekezo hilo kwa Baraza Kuu (NEC) ya chama hicho, na asassi nyinginezo kuu, ili lijadiliwe.

“Chama chetu kinafaa kualika wale wote wanaotaka kuwania ugavana kisha wafanyiwe mahojiano mbele ya jopo maalum litakaloongozwa na kiongozi wetu Raila Odinga.

Jopo hilo litawauliwaza watu hao kuhusu mipango waliyonayo kwa kaunti zao. Baadaye mgombeaji aliyepita ndiye atapewa tiketi ya ODM kushindana na wengine kutoka vyama pinzani katika uchaguzi mkuu,” akasema Bw Wandayi.

Akaongeza: “Wale ambao wataachwa nje wanaweza kugombea nyadhifa zingine kwa udhamini wa vyama pinzani au wanaweza kuamua kuunga mkono chaguo la ODM.”

Pia Bw Wandayi anataka mahojiano hayo ya wagombeaji wa ugavana yafanywe mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti mwaka wa 2022, ili kutoa nafasi kwa kampeni.

“Kufikia Agosti 20121, ODM inapasa kuwa imetambua wagombeaji wake wa ugavana katika kaunti zote nchini,” akasema baada ya kuhudhuria ibada katika Kanisa Katoliki la Rang’ala.

 

Udanganyifu

Mbunge huyo anasema katika miaka iliyopita udanganyifu umekuwa ukikumba mchujo wa chama hicho, haswa kwa viti vya ugavana, na kusababisha migawanyiko siku chache kabla ya uchaguzi mkuu.

“Ghasia pia zimeshuhudiwa katika shughuli hizo, hali ambayo imeiharibia sifa chetu machoni pa Wakenya,” Bw Wandayi akasema.

Akaongeza : “Baada ya mchujo wagombeaji wetu wamekuwa wakikabiliana na watu wale wale walioshindana nao katika mchujo, lakini wapeperusha bendera za vyama vingine.

Hali hii husababisha uharibifu wa rasilimali kando na kupalilia uhasama miongoni mwa wafuasi wetu.” “By 2021 August, ODM should have known their governorship candidates across all the counties in Kenya,” said Mr Wandayi.

Lakini Bi Wanga anashikilia kuwa wagombeaji wote sharti wakabiliane katika kura ya mchujo.

“Ni wajibu wa ODM kuhakikisha kuwa zoezi hilo linaendeshwa kwa njia huru na wazi pasina kuwepo kwa fujo au mapendeleo,” akasema.