• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Lissu, Zitto Kabwe wakaa ngumu, waahidi kushirikiana

Lissu, Zitto Kabwe wakaa ngumu, waahidi kushirikiana

Na THE CITIZEN

DAR ES SALAAM, Tanzania

VYAMA vya upinzani nchini Tanzania vinaonekana vimepuuza barua kutoka kwa afisi ya Msajili wa Vyama (ORPPS) ambayo iliwaonya kwamba ushirikiano kati ya vyama vya siasa kwa sasa unakiuka katiba na sheria za uchaguzi.

Hii ni baada ya mgombeaji wa Urais Kisiwani Zanzibar kwa tiketi ya ACT-Wazelendo Maalim Seif kutangaza kwamba atamuunga mkono Mwaniaji wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( Chadema) Tundu Lissu katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Hapo jana, Kinara wa ACT-Wazalendo Zitto Kabwe, alitangaza akiwa kwenye mkutano wa kampeni mjini Tabora kwamba wataendelea na ushirikiano na Chadema na watatoa tangazo rasmi kuhusu hatua hiyo mnamo Oktoba 3. Siku hiyo chama hicho kitaanda mkutano mkubwa katika uwanja wa Mwembe Yanga, jijini Dar es Salaam.

Lissu aliwahi kunukuliwa akitangaza kwamba anamuunga mkono Kabwe kuwania kiti cha ubunge cha Tabora.

Mnamo Jumanne wiki hii, Naibu Msajili wa vyama vya kisiasa nchini Tanzania Sisty Nyahoza alisema vyama vingeunda miungano yao kufikia makataa ya Agosti 25 na inayoundwa kwa sasa haitambuliki kisheria na ni kinyume cha sheria za afisi yake.

“Tumeandikia ACT-Wazalendo na Chadema tukitaka ufafanuzi kuhusu kauli zilizotolewa na wawaniaji wao Kisiwani Zanzibar na Tanzania bara ambapo viongozi wao walitoa kauli zilizoashiria kwamba wanashirikiana kabla ya uchaguzi mkuu ujao,” akasema

Kulingana naye, afisi yake vilevile iliandikia Katibu wa Chama cha Leba (TLP) na kutaka jawabu baada ya TLP kutangaza kwamba kitamuunga mkono Rais wa John Magufuli anayetetea wadhifa wake kupitia CCM kwenye uchaguzi huo wa Oktoba 28.

Katibu wa TLP Richard Lyimo alithibitisha kwamba alipokea barua kutoka kwa ORPPS hasa baada ya wawaniaji wa chama chake kutumia mabango yenye picha za Rais Magufuli.

“Tulimwandikia barua kuhusu picha hizo na kumweleza uamuzi wa kumuunga mwaniaji wa CCM uliafikiwa wakati wa Kongamano la chama chetu mnamo Mei 9, 2020,” akasema Lyimo.

Hata hivyo, alifafanua kwamba uamuzi huo haukuafikiwa kwa ushirikiano na CCM kwa kuwa wao walikuwa tu na nia ya kumvumisha Rais Magufuli kama mtu binafsi kutokana na utendakazi wake wa kupigiwa mfano kwa muda wa miaka mitano iliyopita.

“Tutaondoa mabango ya wawaniaji wetu yenye picha za Rais Magufuli iwapo afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa itatuamrisha hivyo,” akaongeza.

Katibu wa Chadema John Mnyika hata hivyo aliahidi kuzungumzia masuala hayo baadaye huku wadadisi wengi nao wakiona ushirikiano kati ya ACT-Wazalendo na chama hicho kama tishio kwa uwanizi wa Rais Magufuli.

Hata hivyo, baadhi ya mawakili na wadadisi wa masuala ya kisiasa wamekosoa uamuzi wa afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa, wakisema sheria inasisitiza kuhusu ushirikiano rasmi na wa moja kwa moja badala ya maelewano kati ya wawaniaji wa vyeo mbalimbali.

“Kwa kuwa TLP na UDP ndizo zilikuwa vyama vya kwanza kuunga mkono CCM, kwa nini kuna kasoro upinzani ukiungana?” akauliza mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwanasheria Dkt James Jesse.

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Sheria cha Tanganyika John Seka naye aliunga mkono ushirikiano kati ya vyama vya kisiasa akidai afisi ya msajili imeonyesha wazi kwamba inapendelea CCM.

Profesa Bakari Mohamed ambaye ni msomi wa sayansi ya siasa na mhadhiri wa miaka mingi, naye alisema hakuna sheria inayozuia vyama vya kisiasa kutokuwa na ushirikiano usiokuwa rasmi.

Mwaniaji wa Urais wa Sauti ya Umma Leopold Mahona alisema idara mbalimbali za serikali zinatumiwa kuwakandamiza wawaniaji wa vyama vingine wasiomuunga mkono Rais Magufuli.

You can share this post!

Sababu za Olunga kukosa mechi nne zijazo za Harambee Stars

Wanafunzi wanaosomea udaktari washauriwa kurejea chuoni MKU...