COVID-19: Wagonjwa 13 wafariki idadi jumla ya walioaga dunia nchini Kenya ikigonga 682
Na CHARLES WASONGA
WAGONJWA 13 zaidi wamefariki kutokana na Covid-19 huku visa 218 vipya vya maambukizi ya ugojwa huo vikinakiliwa nchini ndani ya saa 24 zilizopita.
Kulingana na taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, ongezeko hilo la maambukizi limefikisha 37,707 idadi jumla ya maambukizi nchini kufikia Ijumaa.
Na idadi jumla ya watu waliofariki imefika 682 baada ya wagonjwa hao 13 kufariki.
Visa hivyo 218 vipya vya maambukizi viligunduliwa baadsa ya sampuli 5,424 kupimwa na hivyo kufikisha 532,729 idadi jumla ya sampuli ambazo zimepimwa tangu kosa cha kwanza cha Covid-19 kilipogunduliwa nchini.
Visa vipya ya maambukizi vilipatikana katika kaunti zifuatazo; Nairobi (visa 68), Kisii (28), Mombasa (21), Kisumu (19), Kiambu (13), Kajiado (11), Busia (10), Machakos (8), Tharaka Nithi (6), Garissa (6), Taita Taveta (5), Nakuru (4), Uasin Gishu (3), Narok (2), Laikipia (2), Kakamega (2), Kericho (2) na Homa Bay kisa kimoja.
Bw Kagwe pia ametangaza kuwa wagonjwa 170 wamethibitishwa kupona kutokana na Covid-19 na hivyo kufikisha idadi jumla ya waliopona kufika 24,504.
Miongoni mwao, 79 walikuwa wakihudumiwa chini ya mpango wa kuuguzwa nyumbani huku 91 wakiwa ni wale ambao walikuwa wamelazwa katika vituo kadha vya huduma za afya kote nchini.