• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wabunge Omboko Milemba na Johanna Ng’eno waongoza katika orodha ya utendakazi

Wabunge Omboko Milemba na Johanna Ng’eno waongoza katika orodha ya utendakazi

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Emurua Dikirr Johanna Ng’eno ambaye anakabiliwa na kesi ya uchochezi mahakamani ameibuka kuwa wa pili bora katika utendakazi miongoni mwa wabunge wote 290.

Katika matokeo ya utafiti uliondeshwa na kampuni ya Infotrack yaliyotolewa Jumapili, Septemba 27, mbunge huyo alichaguliwa bungeni kwa chama cha Kanu, alipata asilimia 71.4 ya alama zote.

Aliorodheshwa nyuma yake mwenzake wa Emuhaya Omboko Milemba, anayehudumu muhula wa kwanza, aliyepata asilimia 75.4 ya alama.

Walimu wengine walioorodhesha miongoni mwa tano bora ni mbunge wa Mwala Vincent Musyoka (asilimia 70.8) Christopher Aseka wa Khwisero (asilimia 70.0) na Mbunge wa Kibwezi Magharibu Patrick Mweu Musimba (asilimia 69.8).

Wengine walioorodheswa miongoni mwa wachapa kazi bora ni Peter Lochapapong (Sigor), David Pkosing (Pokot Kusini), Robert Mbui (Kathiani), Benjamin Jomo Washiali (Mumias Mashariki) na Erustus Nzioka (Mbooni).

Mkurugenzi Mkuu wa Infotrak Angela Ambitho alisema licha kwamba wabunge 30 bora waliandikisha alama bora, kwa wastani kiwango cha utendakazi wa wabunge kilipungua kutoka asilimia 60 mnamo 2015 hadi asilimia 52.5 mwaka huu wa 2020.

“Kiwango cha wananchi kuridhika na utendakazi wa wabunge kimeshuka sasa ikilinganishwa na bunge la 11. Hii ni ishara kuwa Wakenya wanataka wabunge wa kutia bidii,” akasema Bi Ambitho alipotoa matokeo hayo.

Mkurugenzi huyo mkuu alisema wabunge walioandikisha alama za juu walifanya hivyo kutokana na mchango wao katika utungaji sheria bunge, matumizi mazuri ya fedha za hazina maendeleo (CDF), uzinduzi wa miradi ya maendeleo na namna ambavyo wanashughulikia mahitaji ya wakazi wa maeneo bunge yao,” akaeleza.

Jumla ya Wakenya 37,600 kutoka maeneo bunge yote 290 na wadi 1450 walihojiwa katika utafiti huo ulioendeshwa kati ya Novemba 2019 na Januari 2020.

Wabunge wengine waliorodhesha miongoni mwa 30 bora kwa utendakazi ni pamoja na mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi, James Nyikal (Seme), Didmus Barasa (Kimilili), James Kamau (Kabete), Mark Nyamita (Uriri), Hillary Kosgei (Kipkelion Magharibi).

Wengine ni mbunge wa Kibra Imran Okoth, Joseph Limo (Kipkelion Mashariki), Raymond Moi (Rongai), Swarup Mishra (Kesses), Joshua Kandie (Baringo ya Kati), Benjamin Dalu (Kinangop), Christopher Nakuleu (Turkana Kaskazini), Victor Munyaka (Machakos Mjini), Raphael Wanjala (Budalang’i), Joshua Kimilu (Kaiti), Daniel Maanzo (Makueni), John Munene (Kirinyaga ya Kati), Alfred Keter (Nandi Hills), Khatib Mwashetani (Lungalunga).

Naye marehemu Suleiman Dori anafunga orodha ya wabunge 30 wachapa kazi kwani alifariki mnamo Machi 26, 2020 baada ya utafiti kukamilishwa.

Mbunge wa Isiolo Kusini Abdi Tepo ambaye juzi alifurushwa na waombolezaji katika eneo bunge lake, ndiye anashikilia nambari ya mwisho kwa kuandisha kiwango cha uridhishwaji wa asilimia 33 pekee.

Kati tapo la Wabunge Wawakilishi wa Wanawake, Rosa Buyu wa Kisumu ndiye aliibuka kidedea kwa kupata asilimia 61.5 za alama zote, akifuatwa kwa karibu na mwenzake wa Homa Bay Gladys Wanga aliyepata asilimia 61.

Mbunge Mwakilishi wa Lamu Ruweidha Obbo alikuwa nambari tatu kwa kupata asilimia 60 huku mwenzake wa Samburu Maison Leshoomo na Rose Museo wa Makueni wakipata asilimia 59.1 na asilimia 57.6 mtawalia.

Mbunge Mwakilishi wa Kiambu Gathoni wa Muchomba ndiye anavuta mkia katika tapo hili la wabunge kwa kuandikisha asilimia 39 za alama zote.

Hii hapa orodha kamili:

You can share this post!

Wataka Sh120,000 kwa kila ng’ombe aliyegongwa na gari

Himizo adhabu ya kiboko irejeshwe kukabili utundu shuleni