• Nairobi
  • Last Updated March 18th, 2024 8:55 PM
Hasara maziwa mawili yakizamisha ardhi

Hasara maziwa mawili yakizamisha ardhi

Na FLORAH KOECH

IDARA za serikali na za kibinafsi katika Kaunti ya Baringo, zinakadiria hasara ya mamilioni ya pesa baada ya miradi ya mijengo kumezwa kabisa na maji yanayoendelea kuongezeka katika Maziwa Baringo na Bogoria.

Maziwa hayo mawili yameongezeka kwa kiwango kikubwa tangu Machi mwaka huu, ikizamisha mijengo ikiwa ni pamoja na taasisi, hoteli, nyumba, hospitali na barabara.

Katika Ziwa Baringo, zaidi ya nyumba nne za wafanyakazi katika uhifadhi wa wanyamapori Ruko zilizojengwa mapema mwaka huu na serikali ya kaunti kwa ushirikiano na na Northern Rangelands Trust (NRT) sasa ziko ndani ya ziwa.

Mkurugenzi wa NRT kaunti ya Baringo Aloise Naitira, alisema mradi huo wa Sh1.5 milioni ambao ungekuwa nyumba ya walinzi wanne katika uhifadhi ulianzishwa mnamo Aprili mwaka huu na ulikuwa katika hatua yake ya mwisho kukamilika.

“Tayari tulikuwa tumekamilisha ujenzi wa nyumba hiyo yenye vyumba vinne ambayo ilikuwa na malazi ya walinzi wetu wanne. Tulitaka kugawanya vyumba mwezi uliopita tu kumezwa na ziwa. Tunavyozungumza sasa imezama urefu wa mita mbili ndani ya maji,” akasema Bw Naitira.

Katika Kipkimbirwo polytechnic mita chache kutoka Ziwa hilo, zaidi ya vyumba vinne ambavyo vingetumika kama madarasa, vyumba vya wafanyikazi na ofisi vimezama kabisa.

Msimamizi wa wadi ya Saimo, Bw Soi Elijah Argut alisema mradi huo wa Sh3.5 milioni ambao ulianzishwa katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 ulikuwa umekamilika kabisa na tayari ulikuwa umeunganishwa na umeme.

“Tulikuwa tukingoja tu kuandikisha wanafunzi mapema mwaka huu tu lakini tukaingiliwa na kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19. Jengo hilo sasa limezama kabisa katika ziwa,” akasema Bw Argut.

Zahanati katika kituo cha biashara cha Kampi Samaki pia imezama kabisa na kuongezeka kwa viwango vya maji katika Ziwa ambalo sasa liko juu ya paa.

Katika kijiji cha Loruk, kidimbwi cha kuosha mifugo cha Sh1.8 milioni ambacho kilijengwa na kitengo cha ugatuzi mnamo 2016 pia kimezama.

Hali sio tofauti katika Kiserian, upande wa Kaskazini mwa Ziwa ambapo mjengo wa Sh3 milioni uliojengwa na serikali ya kaunti mnamo 2017 pia ulimezwa na maji ya mafuriko.

Kulingana na mkurugenzi wa kaunti ya Baringo anayesimamia uvuvi, Bw Morphat Okeyo, mradi ambao ulitumika kama pwani ya kutua sasa umezama kabisa na sehemu fulani ya paa hiyo inaonekana kidogo ndani mwa ziwa hilo.

“Nyumba kuu ilikuwa imekamilika kwa gharama ya Sh3 milioni na kazi pekee zilizokuwa zimebaki ni ujenzi wa ua na vyoo. Jengo hilo ambalo lilimezwa miezi mitatu iliyopita sasa ni takriban kilomita moja ndani ya ziwa, ”akasema Bw Okeyo.

Katika Ziwa Bogoria, lango kuu ambalo lilijengwa katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018 na serikali ya kaunti ikiwa ni pamoja na maafisi pia liko ndani ya ziwa.

Msimamizi wa hifadhi ya kitaifa ya wanyama pori ya Bogoria James Kimaru alibaini kuwa miradi hiyo miwili ilijengwa kwa gharama ya Sh30 milioni.

Kulingana na msimamizi huyo, kilomita 26 ya barabara ya Loboi-Emsos ndani ya hifadhi ya wanyamapori inayoelekea kwenye chemchemi za moto, zilizojengwa kwa gharama ya sh15 milioni pia zimezama asilimia 80 kwa maji.

“Baadhi ya maduka ya curio karibu nayo yaliyojengwa kwa Sh2 milioni na maeneo ya kambi ya Sh3 milioni ndani ya hifadhi hayakuokolewa pia. Tumepoteza miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh57.5 milioni na inatarajiwa kuongezeka iwapo viwango vya maji vitaendelea kuongezeka,” akasema Bw Kimaru.

Taifa Leo ilibaini kuwa zahanati ya Loboi iliyojengwa kwa Sh40 milioni ambayo hapo awali ilikuwa kilomita mbali na ziwa sasa iko ndani kwa kilomita mbili.

Mlinzi wa Ziwa Baringo Jackson Komen alisema Ziwa hilo limeongezeka kwa zaidi ya asilimia 80 tangu mvua ilipoanza Machi. Watu zaidi ya 10,000 wamelazimika kuhama makwao.

You can share this post!

Ubinafsi unavyowasukuma wanasiasa kumezea mate Ikulu huku...

Mbunge akamatwa kwa kuchochea maandamano