MANAHODHA WA DOMO DOMO
NA AHMED MOHAMED
WANASIASA wakuu wanaomezea mate kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022 wameanza kampeni za mapema, miaka miwili kabla ya shughuli hiyo, huku wakitoa ahadi ambazo wamekuwa wakirudia kila msimu wa uchaguzi lakini hawazitimizi wanapoingia madarakani.
Hii inatokea wakati Kenya inapokabiliwa na matatizo mengi zikiwemo athari za Covid-19, mzigo mkubwa wa madeni, ufisadi, umaskini, ukosefu wa ajira, mfumo duni wa afya, ushuru wa juu kupindukia na migawanyiko ya kikabila.
Wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM Raila Odinga na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka, wanasiasa hao wameanza kutoa ahadi za kutatua matatizo yaliyopo iwapo watakuwa marais, badala ya kuongoza kutafuta suluhisho sasa.
Tabia hii ya kampeni za mapema na ahadi hewa imekuwa ikishuhudiwa nchini kila mara, lakini wengi wanapochaguliwa hupuuza maslahi ya raia, na badala yake kuangazia yao ya kibinafsi na ya washirika wao wa kisiasa na kibiashara.
Kulingana na Bw Philip Mbaji, ambaye ni mchanganuzi wa siasa eneo la Pwani, wanasiasa hao wamekuwa wakirudia ahadi ambazo walitoa tangu walipoanza siasa na nyingi hawajatimiza.
Bw Mbaji anasema wananchi wanataka kupata suluhisho sasa kwa shida zinazowakumba na sio ahadi ambazo zimekuwa zikipeanwa miaka nenda miaka rudi: “Wakati huu watu hawataki ahadi za bure. Huu sio wakati wa kupiga siasa bali viongozi wanafaa kushikana na kutatua shida za wananchi. Watu wanapitia shida nyingi wakati huu na huwezi kuwaambia wangoje hadi 2022,” akasema Bw Mbaji.
Vigogo hao wamekuwa wakiandaa mikutano ya hadhara kuonyesha ubabe wa kuvuta umati huku wakieneza bila aibu ahadi ambazo wamekosa kutimiza kwa miaka na mikaka licha yao kuwa na uwezo huo serikalini.
Dkt Ruto, ambaye ndiye ameonekana kufanya ziara nyingi zaidi kitaifa, anatumia umaskini uliovuka mipaka nchini, hasa miongoni mwa vijana, kuwavutia walalahoi kwa ahadi kuwa ana suluhisho la kubuni mamilioni ya nafasi za kazi na mbinu nyingine za kuwasaidia kujiinua kimaisha.
KUTEKA HISIA ZA WALALAHOI
Katika kuafikia hili, Dkt Ruto amekuwa akiwatembelea na kutangamana nao maeneo yao ya uchochole akilenga kuteka hisia zao ili wamchukulie kama mmoja wao na anayeelewa matatizo yanayowakumba.
Hii ni licha yake kuwa Naibu Rais tangu 2013, na katika kipindi hicho cha miaka minane hajaonyesha msukumo wa kutetea masuala ambayo anajipigia debe atazingatia akichaguliwa rais.
“Kabla ya kuzungumzia kuhusu ugawanaji madaraka, tuanze kwa kumpa nguvu za kifedha mama mboga, kinyozi, bodaboda, bebabeba, jamaa wa mkokoteni…” amekuwa akisema.
Kabla ya kuwa Naibu Rais alihudumu katika wizara kadhaa akiwa waziri, naibu waziri na pia mbunge.Bw Odinga naye alikuwa waziri mkuu kati ya 2008 na 2013 na kwa sasa ni mwandani wa Rais Kenyatta, hivyo kumpa ushawishi wa kuboresha maisha ya Wakenya kwa wakati huu kuliko kungoja hadi awe rais 2022.
Alipokuwa waziri mkuu, Bw Odinga hakuonyesha ari ya kusukuma mageuzi yatakayohakikisha sera bora za kubuni ajira na kupigana na umaskini, hivyo hajadhihirisha umakinifu wa kukwamua wananchi wa kawaida kutokana na matatizo mengi yanayowakumba.
Pia alihudumu akiwa waziri katika utawala wa Mwai Kibaki kati ya 2002 na 2005 na ule wa marehemu Daniel Moi.Kwa upande wake, Bw Musyoka alikuwa makamu wa rais kati ya 2007 na 2013 na waziri kwa miaka mingi katika serikali za marehemu Moi na Mzee Kibaki, kipindi ambacho angetumia kusukuma mageuzi ya kuinua maisha ya wananchi wa kawaida akiwa ndani ya serikali, lakini hakufanya hivyo.
Hatua ya Bw Odinga na Bw Musyoka kupuuza kazi zao kama viongozi wakuu wa upinzani pia inadhihirisha wanasiasa waliokosa misimamo thabiti ya kisiasa baada yao kuamua kushirikiana na serikali ambayo walikosoa sera zake awali.
Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Bw Robby Muhambi, wanasiasa wanaopiga kampeni za mapema wanaona kama walipoteza muda mwingi wakati mikutano ya siasa ilipozimwa kuepusha maambukizi ya virusi vya corona.
“Saa kila mmoja wao analenga kuhakikisha kuwa haachwi nyuma,” akasema Bw Muhambi.
Wiki mbili zilizopita Dkt Ruto alizuru Pwani na kufuatwa na Bw Odinga kabla ya Bw Musyoka kufululiza huko wikendi iliyopita alikokuwa hadi jana.
Katika ziara zao Pwani, watatu hao walidai wanalenga kuleta mabadiliko makubwa kwa wakazi wa Pwani endapo watashinda urais.
Huu ndio umekuwa wimbo wao wa miaka mingi, ambapo wamekuwa wakiahidi kuboresha maisha ya Wapwani hasa kuhusu suala la mashamba, lakini wote watatu huwa wanasahau mara wanapoingia ofisini na kisha kuwakumbuka tena Wapwani uchaguzi unapokaribia.
Mbali na mashamba, Wapwani wamekuwa wakilalamikia kuhamishwa kwa shughuli za bandari hadi Nairobi na Naivasha, jambo ambalo limesababisha maelfu yao kupoteza ajira na biashara kudorora.